
▪️Ni kufuatia wito wa serikali wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya madini
▪️Waziri Mavunde asisitiza kufuatwa kwa matakwa ya sheria juu ya utekelezaji wa miradi ya madini
▪️Kiwanda cha Kusafisha Nickel kujengwa nchini
▪️Uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi unategemewa kufanyika ifikapo Mwezi Oktoba, 2025
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kampuni ya Tembo Nickel Ltd imethibitisha ratiba ya kuanza rasmi ujenzi wa Mgodi wa Kabanga Nickel uliopo wilayani Ngara,Kagera.
Hayo yamesemwa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lifezone Metals inayomiliki kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited kwa ubia na Serikali ya Tanzania, Ndg. Chris Showalter, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kabanga Nickel kufuatia agizo lililotolewa na serikali la kutaka kampuni zote zenye Leseni za uchimbaji madini wa kati na kubwa kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa miradi husika baada ya kupata Leseni za uchimbaji Madini.
“Kampuni ya Tembo Nickel inathibitisha uendelezaji wa mradi wa Kabanga Nickel kwa mpango wa kuanza na uzinduzi rasmi wa ujenzi wa mradi(𝙜𝙧𝙤𝙪𝙣𝙙𝙗𝙧𝙚𝙖𝙠𝙞𝙣𝙜 𝙘𝙚𝙧𝙚𝙢𝙤𝙣𝙮) ifikapo mwezi Oktoba,2025.
Sambamba na ujenzi wa mgodi huo,Kampuni inaendelea kuthibitisha mpango wake wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusafisha madini ya Nickel kwa kuyaongezea thamani ndani ya nchi”Amesema Showalter

Akizungumza katika kikao hicho,Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema Mradi wa Kabanga Nickel ni mmoja ya miradi mikubwa ambayo inategemewa kuleta mapinduzi makubwa katika kuchochea uchumi na maendeleo ya nchi yetu,hivyo “𝙘𝙤𝙢𝙢𝙞𝙩𝙢𝙚𝙣𝙩” iliyowekwa na Kampuni ya utekelezaji wa mradi ni muhimu kwa mustakabali ya ukuaji wa sekta ya madini na uchumi wa nchi.
Serikali imetoa wito kwa kampuni zote kuhakikisha zinaanza mara moja shughuli za uendelezaji miradi ya madini kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya madini sura ya 123, ni muhimu sheria kuzingatiwa katika utekelezaji wa miradi ili miradi hii ilete tija kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde amesisitiza Kampuni zote zenye Leseni za kati na kubwa kuhakikisha maeneo yao yanaendelezwa kwa mujibu ya masharti ya Leseni zao.







No comments:
Post a Comment