MAADHIMISHO YA SIKU YA UTUMISHI WA UMMA 2025 KUFANYIKA VIWANJA VYA CHINANGALI, DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 28, 2025

MAADHIMISHO YA SIKU YA UTUMISHI WA UMMA 2025 KUFANYIKA VIWANJA VYA CHINANGALI, DODOMA


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomiu
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Mei 28,2025, kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yatafanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni 2025


Na Okuly Julius,DODOMA


Serikali imetangaza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yatafanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni 2025, yakihusisha maonesho ya kazi na utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, amesema maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.”

Katika maonesho hayo, taasisi za umma kutoka ngazi mbalimbali zitatoa huduma mbalimbali kwa wananchi papo kwa hapo, zikiwemo usajili wa vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, pamoja na huduma za afya kutoka hospitali mbalimbali zikiwemo Benjamin Mkapa, JKCI, MOI na Muhimbili. Pia kutakuwepo na huduma ya Gazeti la Serikali.

“Siku ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya mataifa yao na bara kwa ujumla,” amesema Bw. Mkomi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, shughuli za maadhimisho hujumuisha maonesho ya kazi, utoaji wa elimu kwa umma, na majadiliano ya kitaalamu yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya umma.

Mkomi amebainisha kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa taasisi za umma kuonesha ubunifu wao, kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi na kubadilishana uzoefu wa kitaasisi.

Aidha, Bw. Mkomi alitumia fursa hiyo kuwasihi watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

“Watumishi wa umma wana wajibu wa kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kuhakikisha wanasajiliwa na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu ujao,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment