Ujenzi wa miundombinu ya Barabara yarahisisha usafiri kwa wananchi Mtumba - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 8, 2025

Ujenzi wa miundombinu ya Barabara yarahisisha usafiri kwa wananchi Mtumba



Na. Leah Mabalwe, MTUMBA


Kata ya Mtumba yanufaika na ujenzi wa barabara pamoja na kalavati kwa gharama ya shilingi 73,000,000 kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.

Hayo yalielezwa na Diwani wa Kata ya Mtumba, Edward Maboje alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo kuona miradi ya maendeleo mbalimbali iliyotekelezwa na serikali kwa kipindi cha miaka minne.

Diwani Maboje alisema kuwa kata yake imepata miundombinu mizuri ambayo inasaidia usafiri kupatikana kwa urahisi.

“Katika kata hii ya Mtumba tulikuwa na changamoto ya ubovu wa barabara kwa kiasi kikubwa, hususan barabara za Mtaa wa Vikonje pamoja na barabara kutoka Mtumba Kibaoni hadi Shule ya Msingi Mtumba na hali hii ilikuwa ikiwapa changamoto wakazi wa mtaa huo kwasababu hapo mwanzo mvua zilipokuwa zikinyesha watu walikuwa wakipata shida kuvuka na kwenda sehemu nyingine” alisema Maboje.




Aliongeza kuwa wananchi wa Kata ya Mtumba wanafuraha kubwa kupata miundombinu hiyo.

“Serikali imetuletea jumla ya shilingi 73,000,000 kwaajili ya ujenzi wa barabara hizi. Niseme kwamba toka ujenzi huu wa kalavati pamoja na kutengeneza barabara uanze ingawa sio kwa kiwango cha lami imeweza kuwarahisishia wananchi kuvuka na kwenda sehemu nyingine kwaajili ya kufuata mahitaji na hata wasafirishaji wanaweza kusafirisha watu pamoja na bidhaa kiurahisi” aliongeza Maboje.

Kwa upande wake mwananchi Cosmas Kanjongo alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwajengea barabara ambayo inawasaidia kusafiri kwa haraka.

“Kutokana na ujenzi huu wa kalavati pamoja na barabara hapa kwetu, tumesaidika sana. Kwanza kabisa hili kalavati linatusaidia kwa msimu huu wa mvua hatukupata madhara makubwa kwasababu linaruhusu maji kupita kiurahisi kuelekea sehemu zingine. Na hii barabara ilivyoboreshwa inatusaidia kwasababu inapitika kiurahisi, tunaweza kupitisha mizigo yetu kuelekea barabara kubwa” alisema Kanjongo.

Naye Celina Chibada aliipongeza serikali kwa kutatua changamoto ya barabara ambayo imeleta msaada kwa wanawake na watoto wanaotumia barabara hiyo.

“Kabla ya ujenzi huu wa barabara kulikuwa hapapitiki na mvua zilivyokuwa zinanyesha pikipiki zilikuwa hazipiti, sisi wanawake na watoto tulikua tunateseka sana kupita. Kwa sasa tunaishukuru sana serikali kwa kutujengea hii barabara pamoja na kalavati tunanufaika nayo sana” alipongeza Chibada.

No comments:

Post a Comment