
Na. Leah Mabalwe, MTUMBA
Kata ya Mtumba, Halmashauri ya Jiji la Dodoma yapatiwa jumla ya shilingi 83,000,000 kwaajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwainua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Hayo yalielezwa na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mtumba, Huruma Mwigune wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Alisema kuwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri imewawezesha kuendesha maisha na kukuza kipato.
“Katika wanufaika wa mikopo ya asilimia 10, Kata ya Mtumba ni miongoni mwa kata ambayo imenufaika na mkopo wa jumla ya shilingi 83,000,000 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025. Mkopo ulitolewa kwa baadhi ya vikundi vilivyokidhi vigezo na kikundi kimojawapo ni kikundi cha wanawake Ngalawa kinachojishughulisha na ushonaji. Kwa kweli mkopo huu unatunufaisha kwa kiasi kikubwa tumejikita kufanya shughuli mbalimbali tofauti na hapo awali” alisema Mwigune.

Nae mjumbe wa kikundi cha Ngalawa, Monica Petro aliishukuru serikali kwa kuwainua kupitia mikopo ya asilimia 10 inayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha.
“Mikopo hii kwa kweli imetuinua kwa kiasi kikubwa kwa kuendesha shughuli mbalimbali hususan katika familia zetu kwa kujipatia kipato, kipindi cha mwanzo tulikuwa na vishughuli vyetu vidogo vidogo ambavyo tulikuwa tunajichanga changa sisi wenyewe” alishukuru Petro.
No comments:
Post a Comment