VIONGOZI WA UMMA WAJENGEWA UWEZO WA KUIMARISHA UTAWALA BORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 15, 2025

VIONGOZI WA UMMA WAJENGEWA UWEZO WA KUIMARISHA UTAWALA BORA

 


Kukuza maadili ni safari endelevu na hitaji muhimu utumishi wa umma, ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma na kuimarisha utoaji huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 14 Mei 2025, jijini Arusha na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Missaile Musa wakati akifunga mafunzo ya maadili kwa wakuu wa taasisi za umma, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushirikiana na chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kwa lengo la kuwapa uelewa wa kina juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Tunamatarajio makubwa kwamba kama wakuu wa taasisi za umma, mtatumia maarifa na ujuzi mlioupata katika kuleta mabadiliko yanayoonekana na msisitizo mpya juu ya maadili ndani ya taasisi zenu na kuleta matokeo chanya kwa ngazi zote na kuwanufaisha watanzania" Bw. Missaile

Aidha, ameipongeza sekretarieti ya maadili pamoja na IAA kwa kutoa mafunzo hayo na kutoa wito kwa viongozi wengine wa umma hapa nchini kushiriki mafunzo hayo kwa maslahi mapana ya taifa.

Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam-IAA, Dkt. Grace Idinga, amesema chuo kimejizatiti kushirikiana na taasisi na mashirika ya umma kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha utendaji na uadilifu wa viongozi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za chuo katika kuchangia maendeleo ya kitaifa kupitia elimu na mafunzo bora.

Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili Kanda ya Kaskazini, Gerald Mwaitebele, amesema Mafunzo hayo yanalenga kuhakikisha viongozi wa umma wanakuwa na uelewa wa kina kuhusu maadili na uwajibikaji, huku akiwataka washiriki kuwa mabalozi katika maeneo yao ya kazi, wakihimiza uwazi na uwajibikaji kwa vitendo.

Piencia Kiure, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ameeleza kuridhishwa kwake na maudhui yaliyotolewa, akibainisha kuwa yamempa uelewa mpana wa masuala ya maadili na kumjengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za ukiukwaji wa maadili katika maeneo ya kazi.

Mafunzo haya ya muda mfupi kuhusu maadili na uadilifu kwa viongozi wa umma, yanaendelea maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tunguu - Zanzibar, Mwanza, Tanga, Dar es Salaam na Karatu.



No comments:

Post a Comment