AFRIKA IPEWE UHURU WA KUZALISHA NISHATI KWA KUTUMIA RASLIMALI ZAKE: DKT. BITEKO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 19, 2025

AFRIKA IPEWE UHURU WA KUZALISHA NISHATI KWA KUTUMIA RASLIMALI ZAKE: DKT. BITEKO



Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa nchi za Afrika kupewa uhuru wa kuzalisha nishati kwa kutumia raslimali zilizopo barani humo.

Dkt. Biteko ametoa wito huo leo Juni 19, 2025 wakati akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linalofanyika nchini Urusi.

Amesema Afrika inahitaji programu itakayosaidia kufikia dhamira yake ya kuondoa idadi kubwa ya watu ambao hawatumii nishati safi huku akitaja baadhi ya athari za matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo uharibifu wa mazingira.

Ameongeza kuwa Afrika ina vyanzo vingi vya kuzalisha nishati, mfano Tanzania kuna vyanzo kama vile jua, maji na gesi asilia. Hata hivyo barani humo hakuna uhuru wa kutumia makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa kiwango kikubwa pamoja na kuwa nchi kubwa duniani zinaweza kufanya hivyo.

“ Hivyo iangaliwe namna kwa kila nchi kutumia raslimali zake ili kuzalisha nishati, mfumo uliopo unazifanya nchi zote kuwa sawa lakini ukweli ni kwamba hatuko sawa. Kwa mfano Afrika inachangia asilimia 3 hadi 4 pekee ya uchafuzi wa mazingira, lakini imepewa mzigo mkubwa zaidi.” Amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza” Kila nchi itumie utaratibu wake wa kuzalisha nishati lakini kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira.”

Amezungumzia uhusiano mzuri uliopo wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi na kusema kuwa uendelee kuwa wa kuheshimiana na kukubaliana.

Ambapo ametaja manufaa yake kuwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi na kuisaidia Tanzania katika mitaji ya miradi nishati.

Amebainisha kuwa Tanzania ina mpango wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuzalisha takribani megawati 120 za umeme.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Urusi, Mhe. Sergey Tsivilev amesema kuwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Vladimir Putin amekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha zinaungana na nchi zingine katika kupatia ufumbuzi changamoto za masuala ya nishati.

Naye, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya African Energy Chamber, Bw. NJ Ayuk amesema kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika na Urusi kuungana na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika na kutekeleza wanayokubaliana ili wote waweze kunufaika na uhusiano kati yao.

Aidha, ameiomba Serikali ya Urusi kuwezesha kampuni kutoka nchini humo ili ziweze kuwekeza zaidi Afrika hususan katika sekta ya nishati.

Pia, ameipongeza Tanzania katika hatua iliyopiga na mafanikio yake katika sekta ya nishati sambamba na kutoa wito kwa nchi za Afrika kujifunza zaidi kutokana na mafanikio yaliyopo nchini Urusi.

Jukwaa hilo la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg linatarajiwa kuwa na washiriki kutoka takribani nchi 140.





No comments:

Post a Comment