NAIBU WAZIRI KIHENZILE: UCHUKUZI UNAGUSA MAISHA YA KILA MTANZANIA KILA SIKU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 19, 2025

NAIBU WAZIRI KIHENZILE: UCHUKUZI UNAGUSA MAISHA YA KILA MTANZANIA KILA SIKU



Na Hamida Ramadhani – Dodoma


NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), amesema kuwa sekta ya uchukuzi ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayogusa maisha ya kila Mtanzania, kila siku na kila wakati, kutokana na mchango wake mkubwa katika uchumi na ustawi wa wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo, Juni 19, 2025, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Uchukuzi katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Mhe. Kihenzile amesema huduma za reli, barabara, anga na usafiri wa majini ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma, bidhaa na fursa za maendeleo.

"Ziara hii imenipa nafasi ya kusikiliza changamoto za watumiaji wa huduma hizi moja kwa moja, na kuwaelekeza watoa huduma kuratibu maoni hayo ili kuboresha huduma kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya taifa," amesema Naibu Waziri.

Ameongeza kuwa maonyesho haya ni jukwaa muhimu la kujifunza, kutathmini utendaji, na kutambua iwapo taasisi za umma zinatimiza wajibu kwa uadilifu, weledi na ubunifu kwa lengo la kumtumikia mwananchi.

"Tuna wajibu wa kujenga mfumo unaomweka mwananchi mbele, tunapaswa kuhakikisha kuwa kila hatua tunayochukua inaleta tija kwa wananchi wetu," alisisitiza Kihenzile.

Akiwa kwenye ziara hiyo, Mhe. Kihenzile alipokelewa kwa hamasa kubwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi, ambapo walijadiliana kuhusu maboresho ya huduma, uanzishaji wa huduma mpya, mikakati ya usafirishaji endelevu, na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili abiria na waendeshaji.

Ametaja kuwa Wizara ya Uchukuzi inaendelea kuimarisha huduma zake kupitia matumizi ya teknolojia na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara za kisasa, uboreshaji wa bandari pamoja na matengenezo ya meli katika maziwa ya Victoria na Tanganyika.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Katika sekta ya uchukuzi, juhudi zinaendelea kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, salama, kwa gharama nafuu na kwa wakati.




No comments:

Post a Comment