
Bodi ya Kitaifa ya Masuala ya Msaada wa Kisheria, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Saulo Malauri, imekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya kutembelea wadau na watoa huduma za msaada wa kisheria mkoani humo.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano na kupata mrejesho kuelekea kikao cha Bodi hiyo kinachotarajiwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26 Juni 2025 katika Ukumbi wa Chuo cha Uongozi wa Mwalimu Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.
Katika mazungumzo hayo, ambayo yamefanyika leo tarehe 24 Juni 2025 viongozi hao wamejadili utekelezaji wa masuala mbalimbali yahusuyo msaada wa kisheria, ikiwa ni pamoja na changamoto zilizopo, mafanikio yaliyopatikana, pamoja na fursa za kuboresha huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Aidha, wamepokea maoni, mapendekezo na ushauri kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu namna bora ya kuimarisha upatikanaji wa msaada wa kisheria, ikiwa ni pamoja na maboresho ya sera na sheria zitakazowezesha wananchi wengi zaidi kupata haki kwa urahisi, bila kujali hali zao za kiuchumi.
Mapendekezo yatakayokusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali wa mkoa wa Pwani yatawasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, kama sehemu ya mchango wa Bodi katika kuboresha mfumo wa haki na kuimarisha misingi ya utawala wa sheria nchini.





No comments:
Post a Comment