BUNGE LARIDHIA MAREKEBISHO YA MPAKA WA HIFADHI YA TAIFA NYERERE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 26, 2025

BUNGE LARIDHIA MAREKEBISHO YA MPAKA WA HIFADHI YA TAIFA NYERERE



Na Anangisye Mwateba, Dodoma


Bunge limeridhia ombi la Serikali la kumega sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa lengo la kutatua migogoro ya mipaka na kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea katika mazingira rafiki kwa jamii na uhifadhi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana, akiwasilisha azimio hilo bungeni, amesema kuwa Serikali imeamua kumega eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,617 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kulirejesha katika Pori la Akiba Selous.

Amesema hatua hiyo imepunguza ukubwa wa hifadhi hiyo kutoka kilomita za mraba 30,893 hadi kufikia kilomita za mraba 29,276.

Akifafanua zaidi, Mhe. Chana amesema hatua hiyo inalenga kuondoa migogoro ya muda mrefu ya mipaka baina ya hifadhi hiyo, vijiji vinavyoizunguka, Pori la Akiba Selous na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Mbarang’andu, Juhiwangumwa, Iluma, Jukumu, Magingo na Nalika.

“Kwa kufanya hivyo, tunaimarisha usalama wa maeneo yaliyohifadhiwa, tunajenga mahusiano bora kati ya wananchi na hifadhi, na kuondoa migogoro iliyodumu kwa muda mrefu,” amesema Mhe. Chana.

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa marekebisho hayo ya mpaka yanalenga kulinda mfumo ikolojia muhimu unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la Akiba Selous, sambamba na kuhakikisha mtiririko endelevu wa maji katika Mto Rufiji, ambao ni chanzo kikuu cha uzalishaji umeme kupitia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP).

Mhe. Chana amebainisha kuwa hatua hiyo itaongeza tija kwa Taifa kwa kuimarisha shughuli za utalii, uwindaji wa kitalii katika Pori la Akiba Selous na maeneo yanayozunguka, na hivyo kuchangia mapato ya ndani kupitia sekta ya utalii.

“Kwa sasa, tunaelekea katika uboreshaji wa uhifadhi wa maliasili kwa ujumla wake – wanyamapori, mimea, mazalia ya viumbe wa majini na pia kuongeza upatikanaji wa maji kwa matumizi ya wakulima, wafugaji na wavuvi,” ameongeza.

No comments:

Post a Comment