SALOME MAKAMBA AFUNGA MAONYESHO YA NISHATI EXPO 2026 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 25, 2026

SALOME MAKAMBA AFUNGA MAONYESHO YA NISHATI EXPO 2026



Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba leo tarehe 25 Juni, 2026 amefunga rasmi Maonesho na Kongamano la Nishati Safi Expo 2026 yaliyofanyika katika ukumbi wa EACLC jijini Dar es Salaam

Akiwa katika banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ameipongeza REA kwa kuendelea kusambaza na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.


"Naipongeza REA kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuimarisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na naendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kutumia teknolojia mpya za nishati safi ili kulinda afya, mazingira na kuboresha ustawi wa jamii, " Ameongeza Mhe. Makamba.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya Taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia yanafikiwa kwa manufaa ya Watanzania wote.

Aidha, Mhe. Makamba ameelezwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha wananchi wanahama kutoka katika matumizi ya nishati zisizo safi na zisizo salama kwenda kwenye teknolojia bora za nishati safi ya kupikia.

Vilevile, Mha wa miradi Francis Manyama amemfafanulia kuwa kupitia maonesho hayo, REA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuonesha teknolojia mbalimbali ikiwemo matumizi ya kuni mbadala, majiko banifu, majiko ya umeme na teknolojia nyingine rafiki kwa mazingira.

Alieleza kuwa washiriki mbalimbali wakiwemo baba lishe, mama lishe, washiriki kutoka asasi za kirai, na mashirika ya binafisi, walimu na wadau wengine walitembelea banda la REA na kupata elimu pamoja na kujionea teknolojia hizo zinazochochea matumizi ya nishati safi nchini.

Aidha, Mha. Manyama alimueleza Mhe. Makamba kuwa REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo usambazaji wa majiko banifu 200,000 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara pamoja na usambazaji wa mitungi ya gesi ya LPG ya kilo sita ipatayo 3,255 kwa kila Wilaya kwa lengo la kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Vilevile, alibainisha kuwa Wakala unatekeleza mradi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku, ambapo utekelezaji wake unafanyika kwa ushirikiano na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Jeshi la Magereza.

Katika hatua nyingine, alieleza kuwa REA kupitia TPDC imetekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia ya kupikia katika kaya zilizopo mikoa ya Lindi na Pwani, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi na salama kwa wananchi wa maeneo hayo. Pia alieleza kua Wakala kupitia STAMICO utawezesha usimikaji wa mashine ya kuzalisha mkaa mbadala katika mkoa wa Geita ili kurahisha upatikanaji endelevu wa nishati ya kupikia kwa wingi na wakati.



No comments:

Post a Comment