WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUCHANGIA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, June 25, 2026

WAZIRI GWAJIMA ATOA WITO KWA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KUCHANGIA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA 2050


Na Boniphace John, Dodoma


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imesisitiza umuhimu wa mgawanyo sahihi wa majukumu katika ngazi za wilaya, mkoa na taifa ili kuepusha migongano, kuongeza ufanisi na kuimarisha uhalali wa maamuzi.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Uendeshaji wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Toleo la Pili la Juni 2026.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima, alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo ya taifa.

Alisema mashirika hayo yamekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za kijamii, kukuza haki, kusaidia makundi maalum, kujenga uelewa wa wananchi na kushirikiana na Serikali katika kufikia malengo ya maendeleo.

Mhe. Gwajima pia alitoa rai kwa sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuendelea kuwa mshirika makini wa Serikali katika kuimarisha maendeleo jumuishi, hususan kwa kutoa mchango katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Sekta imara ni sekta inayoweza kuzungumza kwa heshima, kushauriana kwa uwazi na kutatua changamoto kwa hekima. Maendeleo ya kweli hujengwa kwa misingi ya uwajibikaji, uzalendo na huduma kwa wananchi,” alisema.

Aliongeza kuwa uzinduzi wa mwongozo huo unaweka bayana dhamira ya sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuwa sekta inayofuata sheria, kujiongoza kwa maadili na kushirikiana na Serikali kwa ustawi wa taifa.

Aidha, ameyataka mashirika hayo kuendelea kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutawala kwa kujenga uwezo wa taasisi zao, kuboresha usimamizi wa taarifa na nyaraka, pamoja na kukuza ushiriki wa makundi maalum.

“Tuendelee kuifanya sauti ya sekta kuwa sauti ya kujenga, kuunganisha na kuleta matumaini kwa wananchi,” alisisitiza Mhe. Gwajima.

No comments:

Post a Comment