
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mhe. Hassan Bomboko, amesema kuwa, shamba la Chama cha Ushirika Uduru Makoa lenye ukubwa wa ekari 358 limepokelewa rasmi na chama hicho baada ya kushinda kesi dhidi ya mwekezaji, Elisabeth Stegmeir.
Akizungumza na wananchi wa eneo la Uduru Makaa, Wilayani Hai, Mhe. Bomboko ameeleza kuwa, hukumu ya kesi hiyo ilitolewa tarehe 28 Mei 2025, baada ya mchakato wa muda mrefu uliodumu tangu mwaka 2022.
Mhe. Bomboko amesema kuwa mwanzo, chama hicho cha ushirika kilimkodisha mwekezaji huyo kwa makubaliano maalum, lakini baadaye mwekezaji huyo alikiuka masharti na kuacha kulipa kodi kwa kipindi cha miaka minne.
“Huwezi kuamua kukaa kwenye eneo la watu kwa miaka minne bila kulipa kodi, ilhali mali hiyo siyo yako. Najua mlikuwa mnasubiri sana hukumu hii, na niwaambie tu: hukumu imetoka, mmeshinda kesi, na sasa huyu mwekezaji anatakiwa kuondoka katika eneo lenu,” amesema Mhe. Bomboko.
Hata hivyo, Mhe. Bomboko amewasihi wananchi kuepuka kuvamia eneo hilo au kufanya fujo, akisisitiza kuwa, shamba ni mali ya chama, lakini taratibu za kisheria lazima zifuatwe ili mwekezaji huyo aondoke kwa amani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za kisheria zikiendelea ili mwekezaji huyo aondoke rasmi na shamba lirudishwe kwa chama.
“Ni ukweli usiopingika kwamba shamba hili ni letu na ni haki yetu – hilo halina mjadala. Tunakamilisha taratibu nyingine ili makabidhiano yafanyike na haki yetu ipatikane. Tumefanya kazi mchana na usiku kuhakikisha shamba hili linarejea mikononi mwa chama,” amesema Mhe. Mafuwe.





No comments:
Post a Comment