
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wafamasia nchini kuendelea kulipa kipaumbele suala la elimu ya matumizi sahihi ya dawa ili kuisaidia jamii kutambua na kuepuka madhara ya matumizi holela ya dawa.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa wa Ufunguzi wa Kongamano la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wafamasia Tanzania unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). Amesema yamekuwepo matumizi mabaya ya dawa kwa baadhi ya wananchi, kama vile matumizi ya dawa pasipo kushauriwa na Daktari, matumizi ya dawa za usingizi kama kilevi, matumizi ya dawa kunenepeshea mifugo pamoja na matumizi ya dawa kukoleza pombe za asili.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasisitiza wanataaluma wote wa famasi kufanya kazi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yao. Ameliagiza Baraza la Famasi kusimamia kwa ukaribu suala hilo ili kuwahakikishia wananchi huduma bora. Pia ametoa rai kwa Vyuo vinavyofundisha taaluma ya famasi kuzingatia maadili katika ufundishaji ili kuzalisha wanataaluma wenye maadili, weledi na ujuzi stahiki.
Aidha, Makamu wa Rais amekemea tabia ya upotevu wa dawa kutokana na wizi, ambapo amesema badala ya dawa muhimu kupatikana kwenye vituo vya afya, hupatikana kwenye maduka binafsi ya dawa yanayomilikiwa na baadhi ya wafamasia. Amewataka wafamasia wanaojihusisha na tabia hiyo kuacha mara moja pamoja na kuviagiza vyombo vinavyohusika kuchukua hatua stahiki kwa wale watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Vilevile, Makamu wa Rais amewasihi wanataaluma wa famasia kuongeza chachu ya kufanikisha mpango mahsusi wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa zilizo salama na zenye ubora katika vituo wanavyofanyia kazi. Amesema lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma ya dawa bila vikwazo.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kushirikiana na Chama cha Wafamasia nchini kuendelea kuwekeza katika tafiti zenye lengo la kutatua changamoto za kiafya katika jamii, hususan tafiti kuhusu miti na mimea mbalimbali ya asili inayojulikana kuwa tiba katika jamii za kiafrika ili kuweza kuiendeleza na kutengeneza dawa kwa kutumia sayansi na teknolojiana kuwezesha kutibu magonjwa kwa ufanisi zaidi.
Pia ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya bustani za miti na mimea dawa (botanical gardens) ili kuihifadhi na pia kuwarahisishia watafiti wa dawa kutekeleza jukumu hilo.
Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wafamasia katika utoaji wa huduma za afya na itaendelea kushirikiana na wataalamu hao ili kutoa huduma bora za dawa nchini.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewasihi Wafamasia kuhakikisha wanashiriki katika kudumisha amani nchini hususani katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwa kutambua kwamba bila amani hakuna shughuli yeyote itayoweza kufanyika kwa ufanisi.
Akimwakilisha Waziri wa Afya katika ufunguzi huo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kutokana na mabadiliko yaliyojitokeza duniani katika ufadhili wa sekta ya afya, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 141.98 kuweza kufidia pengo lililojitokeza katika bidhaa za afya zinazohusiana na Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI pamoja na dawa muhimu zinazohusiana na mama na mtoto.
Amesema sekta ya Afya itaendelea kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania Fadhil Hezekiah amesema Chama hicho kinaipongeza Serikali kwa kuvutia wawekezaji na hivyo kuwezesha uwekezaji katika sekta ya Afya hususani uanzishwaji wa viwanda,vya bidhaa za afya, pamoja na vituo vya Afya binafsi hapa nchini. Amesema tayari muelekeo mzuri unaonekana wakati nchi ikielekea katika kuwa na utalii wa tiba.
Ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Baraza la Famasi kuweka ulazima wa maduka ya dawa muhimu kuwa na mtaalamu wa famasi aliyesomea fani hiyo ili kusaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza katika maduka hayo. Pia chama hicho kimeomba mabadiliko ya muundo kuanzia ngazi ya Wizara ya Afya, Hospitali ya Taifa, Hospitali za Kanda na Mikoa ili kuwa na kurugenzi ya dawa ndani ya Hospitali hizo.
Mkutano huo wa Siku tatu kuanzia tarehe 04 hadi 06 Juni 2025 una kauli mbiu isemayo “Famasia kiini cha Afya kwa Wote, Ubinifu, Uwekezaji na Afya Jumuishi kwa Wote chini ya Uongozi wa Mabadiliko”









No comments:
Post a Comment