MAJALIWA: WAKUU MIKOA HAMASISHENI WANANCHI KUTUMIA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 16, 2025

MAJALIWA: WAKUU MIKOA HAMASISHENI WANANCHI KUTUMIA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA



WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha wananchi kutumia huduma ya kisheria ya Mama Samia ili iwasaidie kutatua changamoto zao za kisheria.

Amesema kuwa juhudi za utoaji haki haziwezi kufikiwa na Serikali pekee bali zinahitaji ushirikiano wa dhati kutoka kwa kila mmoja ikiwemo viongozi, wazazi, jamii, taasisi za dini, mashirika ya kiraia na wananchi kwa ujumla.

Amesema hayo leo Jumatatu (Juni 16, 2025) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Dar es Salaam iliyofanyika kwenye viwanja vya Maturubai Mbagala jijini Dar es Salaam.

“Dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki kwa wakati bila ubaguzi, ili kujenga jamii yenye mshikamano na utawala wa sheria, Kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake, tunaweza kuwa Taifa linalojivunia mfumo wa haki ulio imara, unaoaminika, na unaowalinda raia wote kwa usawa.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania inaendelea kuwa Taifa linaloongozwa kwa kuzingatia haki, usawa na utawala wa sheria kwa kuwa ndiyo msingi wa amani ya kweli na maendeleo ya kudumu.

Amesema kuwa wajibu wa kila mtanzania, taasisi za umma na binafsi, pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuhakikisha juhudi hizo zinaungwa mkono na zinaendelea kuzaa matunda kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kutoa taarifa za uwepo wa vitendo vya ukatili katika jamii kwenye vyombo husika bila uoga. “Pale ambapo mwanajamii anaona, anasikia au anahisi kuna ukiukwaji wa haki, ni wajibu wake kuhakikisha suala hilo linaripotiwa mapema sehemu sahihi”.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa katika utekelezaji wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, wameamua kutumia falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo zimewezesha kwa kiasi kikubwa kuwa na misingi imara ya utawala bora. “Hivyo ni jukumu la muhimu kwa Wizara ya Katiba na Sheria kutekeleza falsafa hii kuhakikisha upatikanaji haki kwa wananchi katika kujenga taifa lenye usawa, amani na maendeleo.”

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Haroun Ali Suleiman amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Kampeni hiyo imetoa msaada wa kisheria kwa wananchi 422,908 ikiwa wanawake ni 209,185 na wanaume 213, 723 katika mikoa yote mitano ya Zanzibar jambo linaloashiria dhamira ya kweli ya kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kupata haki.

“Kampeni hii imekuwa hatua ya kihistoria katika kuhakikisha wananchi wote wanapata haki bila ya kujali hali yao ya kiuchumi, kijamii au kijiografia”

Kwa upande wake, Naibu Kamishani wa Magereza Dkt. Justine Mhimba Kaziulaya amesema kuwa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mashirika ya watoa Huduma za Msaada wa Kisheria imefanikiwa kutoa huduma kwa wafungwa na mahabusu wapatao 15,664 nchi nzima ambapo kati ya hao 2,998 walihudumiwa na 978 kati yao wameweza kupata dhamana na kuachiliwa huru.

Kwa upande wake Rais Chama cha Mawakili wa Serikali Bavoo Junusi amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuasisi kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia baada ya kuona ipo haja ya watanzania masikini na makundi maalum kupata huduma za kisheria bila malipo

“Rais Dkt. Samia na Serikali yake ni makini wasikivu na wanajali maslahi na ustawi wa watanzania, sisi Mawakili tutahakikisha popote kampeni hii inapofika tunashiriki na kuunga mkono ili watanzania wanufaike na kampeni hii”

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Usawa wa Jinsia (UN Women), Bi. Hodan Addou ameipongeza Serikali kwa kuendesha kampeni ya Msaada wa Kisheria kwa kuwa imesaidia kutoa haki kwa wasio na uwezo ikiwemo wanawake pamoja na kukuza uelewa wa Sheria miongoni mwa Watanzania.” Tunafuraha kuwa katika safari hii ya haki iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia”







No comments:

Post a Comment