
Na Okuly Julius - DODOMA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera, amesema Serikali imenufaika kwa kiasi kikubwa na tafiti za kisayansi katika kutatua changamoto za sekta ya afya nchini.
Akizungumza tarehe 11 Juni 2025 katika Ukumbi wa Jiji, Mji wa Magufuli jijini Dodoma, wakati wa Kongamano la Pili la Sayansi ya Afya (UDOM Scientific Conference on Health – USCHe 2025) Dkt. Mahera ambaye alimwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, alieleza kuwa makongamano ya kisayansi ni jukwaa muhimu linalowezesha Serikali kupokea maoni na mapendekezo ya kitaalamu kutoka kwa watafiti na wanazuoni wa ndani ya nchi.
"Makongamano kama haya yanaiwezesha Serikali kuandaa sera na mikakati ya afya inayotegemea ushahidi wa kisayansi. Ni muhimu tafiti hizi zitumike ipasavyo kwa manufaa ya jamii yetu," alisema Dkt. Mahera na kusisitiza matumizi sahihi ya teknolojia katika kukabili changamoto za kiafya.
Kongamano hilo limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa (SoMD) na Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), likiwa ni sehemu ya mikakati ya kukuza tafiti za afya na kuimarisha mchango wa taaluma katika maendeleo ya taifa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, hivyo UDOM ina wajibu wa kuhakikisha inazalisha wataalamu bora kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
"Kongamano la kisayansi lina umuhimu mkubwa kwa taifa. Tafiti zetu zisitumike na mataifa mengine kutengeneza bidhaa na sisi tuje kununua. Ni lazima tuyatumie matokeo ya tafiti kujinufaisha sisi wenyewe," alisema Prof. Kusiluka.
Aliongeza kuwa sambamba na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ni muhimu tafiti zijielekeze pia kwenye ajali za barabarani ambazo zimeendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo katika nchi zinazoendelea.

Kwa upande wake, Dkt. Grace Magembe, Mganga Mkuu wa Serikali na Mwakilishi wa Wizara ya Afya, alisema Wizara itaendelea kushirikiana na vyuo vikuu katika kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatumika moja kwa moja katika uundaji wa sera na miongozo ya afya.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jabir Shekimweri, alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kushiriki na kuunga mkono makongamano ya aina hiyo, akisisitiza kuwa ni muhimu yawe endelevu kwa ajili ya kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali za kiafya zinazoikabili jamii.






No comments:
Post a Comment