RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA SIMIYU NA MWANZA, KUZINDUA DARAJA LA KIGONGO-BUSISI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 11, 2025

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA SIMIYU NA MWANZA, KUZINDUA DARAJA LA KIGONGO-BUSISI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya siku saba katika mikoa ya Simiyu na Mwanza kuanzia Juni 15, 2025, ambapo atazungumza na wananchi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo Daraja la Kigongo-Busisi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma , Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema Rais Samia atawasili mkoani Simiyu Juni 15 na kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo.

“Tarehe 19 Juni, Rais atawasili mkoani Mwanza na atazindua rasmi Daraja la Kigongo-Busisi ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100. Kukamilika kwa daraja hili ni historia mpya iliyoandikwa na Serikali ya Awamu ya Sita,” amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa mara baada ya ziara hiyo ya ndani, Rais Dk. Samia pia amepata mwaliko maalum na atafanya ziara ya kikazi katika nchi ya Msumbiji na Visiwa vya Comoro.


Kuhusu bajeti Kuu ya Serikali Msemaji Mkuu wa Serikali amesema Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji itawasilisha bajeti kuu ya Serikali pamoja na hali ya uchumi wa taifa, ambapo kwa mara ya kwanza, bajeti hiyo itatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani pekee.

“Hii ni bajeti ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Sita na ya kipekee kwa kuwa itatoa mwelekeo wa bajeti ya uchaguzi mkuu. Itakuwa bajeti ya kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza uchaguzi ujao utafadhiliwa kwa fedha za ndani,” amesema Msigwa.

Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kufuatilia bajeti hiyo, akisisitiza kuwa inaonesha mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia.

Katika hatua nyingine, Msigwa amesema Tanzania imeandika historia kwa kupokea gawio la shilingi trilioni 1.28 kutoka kwa mashirika ya umma, ikiwa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika mashirika hayo.

“Hadi sasa, Serikali imewekeza jumla ya shilingi trilioni 86 katika mashirika ya umma. Matokeo ya uwekezaji huu ni kuongezeka kwa gawio ambalo linatarajiwa kuendelea kupanda mwaka hadi mwaka,” amesema.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya matokeo ya utekelezaji wa falsafa ya 4R (Reconcile, Rebuild, Reform, Reimagine) iliyoasisiwa na Rais Samia kwa lengo la kuimarisha taasisi za umma na uchumi wa taifa.


Akizungumzia ujenzi wa Mji wa Serikali awamu ya pili unaoendelea Mtumba, jijini Dodoma, Msigwa alisema utekelezaji wake umefikia asilimia 90, na unagharimu takriban shilingi bilioni 738.9.

Amesema ujenzi huo unahusisha majengo 34, ambapo sita kati yake yamekamilika na kuanza kutumika na wizara husika.

Pia ameeleza kuwa ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 59.1 unaendelea, pamoja na miundombinu ya umeme wa ardhini yenye urefu wa kilometa 42 ambayo imefikia asilimia 59.

“Ufungaji wa kamera za usalama umefikia asilimia 55, na kampeni ya upandaji miti inaendelea ambapo miti 233,000 tayari imepandwa pembezoni mwa barabara na maeneo ya wazi ya mji huo,” ameongeza.


No comments:

Post a Comment