
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi, aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani amri za kimamlaka alizotoa Rais Dornald Trump wa Marekani za kusitisha misaada Tanzania, zilivyoathiri miradi iliyokuwa inaendelea nchini na hatua zilizochukuliwa kukabiliana na hali hiyo, bungeni jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasilino Serikalini, Wizara ya Fedha)
Na. Peter Haule, WF, Dodoma
Serikali imesema kuwa hakuna athari za moja kwa moja za kibajeti kutokana na amri za kimamlaka alizotoa Rais wa Marekani, Dornald Trump za kusitisha misaada kwa Tanzania.
Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi, aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani amri za kimamlaka alizotoa Rais Dornald Trump wa Marekani za kusitisha misaada Tanzania, zilivyoathiri miradi iliyokuwa inaendelea nchini.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali ya Tanzania haikuwa na ushirikiano wa Serikali kwa Serikali kwa masuala ya fedha za miradi ya maendeleo na Serikali ya Marekani kwa kuwa ilikuwa inatumia taasisi zake ambazo zilikuwa zinashirikiana na taasisi za Tanzania.
“Kwa upande wa taasisi zilizokuwa zinapokea fedha kutoka taasisi za Marekani, tayari Serikali imefanya tathmini si tu kwa tamko la Marekani bali kwa mwenendo wote unaohusisha fedha zinazotoka kwa washirika wa maendeleo na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa”, alisema Dkt. Nchemba
Alisema kuwa huko nyuma kulikuwa na fedha za misaada zilizokuwa zinaenda kwenye bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini kwa sasa Serikali inatekeleza miradi ya maendeleo kupitia fedha za ndani kufidia pengo la miradi ambayo bajeti yake ilikuwa inatoka kwa nchi wahisani.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kutokana na yaliyotokea hivi karibuni kuhusu Sera za nje kutoka kwa Wahisani tayari Serikali imepangilia upya matumizi yake kwa bajeti inayoendelea na kupata zaidi ya shilingi bilioni 220 zilizokuwa zinahitajika hasa kwenye maeneo yaliyoonekana kuathirika hususani sekta ya afya ambayo zimepelekwa zaidi ya shilingi bilioni 88 kuendelea na utekelezaji wa miradi.
Alisema kuwa kupitia tathmini iliyofanywa, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo ilikuwa inapata fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo na maisha ya watanzania hayaathiriki kutokana na mabadiliko ya kisera kutoka kwa mbia yeyote wa maendeleo
Akijibu swali la msingi kuhusu namna Serikali ilivyojiandaa kukabiliana na mabadiliko ya Sera za baadhi ya nchi tajiri kulisaidia Taifa kukuza uchumi, Mhe. Dkt. Nchemba alisema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuongeza mapato ya ndani ili kuhakikisha kuwa sehemu kubwa ya bajeti inagharamiwa kwa kutumia mapato ya ndani.
Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa mahitaji ya kibajeti ikiwemo ugharamiaji wa miradi ya maendeleo, Serikali itaendelea kuvutia ushiriki wa sekta binafsi katika ugharamiaji wa miradi ya maendeleo kwa kutumia njia mbadala ikiwemo ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Dkt. Nchemba alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuipunguzia Serikali mzigo wa kukopa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.
No comments:
Post a Comment