“SITAMNYIMA RUHUSA MTUMISHI ATAKAYETAKA KWENDA MASOMONI”- MKURUGENZI MAJALIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 2, 2025

“SITAMNYIMA RUHUSA MTUMISHI ATAKAYETAKA KWENDA MASOMONI”- MKURUGENZI MAJALIWA



Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Ndg. Said Majaliwa amesema hatamzibia riziki ya kwenda masomoni mtumishi yoyote anayetaka kujiendeleza kielimu kwa kuzingatia taratibu za kiutumishi kwa kuwa kila mtumishi ana ndoto yake kimaisha.

Kauli hiyo ameitoa akiwa mgeni rasmi wakati wa sherehe ya kuwapongeza wahitimu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa njia ya huria na masafa ambao hafla yao imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kondoa Irangi.

“Anayetaka kwenda kujiendeleza mlango wangu upo wazi lakini hapa mnielewe vizuri ukienda kujiendeleza ukirudi tegemea kuendelea palepale ili wanafunzi nao wapate kunufaika na kile ulichoenda kusomea maana ukisoma pia mshahara unaongezeka lakini utakuwa na faida hasa pale zinapotokea fursa mbalimbali”. amesema Mkurugenzi Majaliwa

Aidha, amewapongeza wahitimu waliomaliza kwa kuwa, wakati mwingine, si jambo rahisi kwa mtumishi anayepokea mshahara kurudi shule. Hivyo, Mkurugenzi amewataka wakufunzi kuwafuatilia wanafunzi ambao hawajamaliza masomo yao ili wawasaidie kuendelea na masomo.

Hata hivyo, amewaelekeza Maafisa Elimu kupeleka mapendekezo ya shule ambazo zina vyumba vya madarasa vya ziada ili viweze kutumiwa na wanafunzi hao wa Elimu ya Watu Wazima kwa ajili ya kutatua changamoto yao ya kukosekana kwa vyumba vyenye utulivu kwa ajili ya kusomea. Vile vile, Mkurugenzi ameahidi kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kuwajengea darasa.

Kwa upande wake Afisa Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Mji Kondoa Mwalimu Lucy Mbolu amewapongeza wahitimu na kuwahimiza kwenda kutumia elimu waliyoipata kuonyesha utofauti wa ufanisi katika utendaji kazi wao wa kabla na baada ya kuhitimu masomo.

Wahitimu wamewashukuru wakurugenzi wa Halmashauri hizo mbili, kwa kuwaruhusu kusoma, kufanya mitihani pamoja na mazoezi. Vile vile, wahitimu wamewashukuru viongozi wengine waliowatia moyo wa kusoma na kuwapa maelekezo mbalimbali ambayo yamewasaidia nao kuhitimu na kufikia ndoto zao na kuwaasa wenzao ambao hawana stashahada kujiendeleza kwa kutumia mfumo wa masafa.

Jumla ya wahitimu 61 wamehitimu kati ya wanafunzi 75 waliodahiliwa mwaka 2023 katika kituo cha walimu Iboni wakiwa ni walimu kutoka Halmashauri hizo mbili za wilaya ya Kondoa. Aidha, sherehe hiyo, pia imehudhuriwa na wakufunzi wa kituo hicho.

No comments:

Post a Comment