
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kulinda na kudumisha amani nchini ili kuhamasisha maendeleo na kuziba mianya ya kuibuka kwa migogoro miongoni mwa wanajamii.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili Juni 29, 2025) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufunga kongamano la Afrika Mashariki la Amani lililoandaliwa na The Islamic Foundation, katika viwanja vya shule ya msingi Mirongo jijini Mwanza
“Nataka niwaambie bila amani hatuwezi kupata mafanikio yoyote, kupitia kongamano hili mmepata nafasi ya kujadili kuhusu tunu hii ya amani, ambayo wakati wote tumeshuhudia viongozi wa dini mkiwa kwenye majukwaa yenu mkihimiza amani miongoni mwa wanajamii, tuishike tunu hii”.
Kadhalika, amewataka Watanzania kuangalia kwa upana wake suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii hasa kwa vijana. “Ni muhimu sana suala hili mkaliweka kama agenda katika mikutano na vikao vyenu, kila kiongozi wa dini anapozungumza, suala la maadili na mmomonyoko wa liwe ni ajenga ya kudumu”
Amesema kuwa mabadiliko ya teknolojia na kuiga tamaduni za mataifa ya nje imekuwa miongoni mwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili. “Siku hizi vijana kuwaita wazee kwa majina yasiyo na heshima ni kitu cha kawaida, viongozi ndio wenye jukumu la kusimamia eneo la maadili, mkifanya hivyo tupata vijana wenye maadili mema”
Pia Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa falsafa ya 4R ya Resilience (Ustahimilivu), Reconciliation (Maridhiano) and Reforms (Mageuzi), Rebulding (Kujenga upya) iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi imara ya kulinda amani. “Falsafa hii imeifanya Tanzania kuwa tulivu na salama”
Wakati huo huo Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jamii inapaswa kuona umuhimu wa kukuza utamaduni wa majadiliano na maridhiano katika kushughulikia tofauti zilizopo mingoni mwa jamii.
“Tunapaswa kujenga jamii inayoheshimu maoni tofauti, na kuhimiza mijadala kwenye majukwaa na kwa nafasi hii viongozi, taasisi na wanajamii mnapaswa kuwa daraja la maridhiano badala ya kuwa vyanzo vya migawanyiko”
Naye Mwenyekiti wa Islamic Foundation Aref Nahdi amesema kuwa taasisi zao zitaendelea kushirikiana na Serikali katika kuijenga Tanzania yenye haki, Amani, usawa, maendeleo na heshima kwa wote.
Aidha, amesema kuwa taasisi hizo zitaendelea kukemea vikali kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa amani, upendo na kuvunja heshima za viongozi wa kitaifa. “Kwa kufanya hivyo inakuwa ni sehemu ya mafundisho ya dini”.




No comments:
Post a Comment