
Chato, Geita
Wananchi wa kata ya Buseresere wilayani Chato mkoani Geita wameeleza kunufaika na ujenzi wa barabara ya Maweni yenye urefu wa km 1.5 kwa kiwango cha changarawe.
Akiongea katika mahojiano maalum Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Chato, Mhandisi Edgar Kidasi ameeleza kuwa kazi zilizofanyika katika eneo hilo ni pamoja na kuchonga barabara, kunyanyua tuta, kumwaga kifusi na kujenga mitaro ili maji yapate uelekeo sahihi kipindi cha mvua.
"Eneo hili lilikuwa korofi hasa kipindi cha mvua na ukizingatia kwamba barabara hii inawasaidia wananchi kufika Hospitali, shuleni na eneo la soko ambapo hapo awali palikuwa hapapitiki lakini sasa wananchi wanapita bila shida yoyote", amesema Mhandisi Kidasi.
Naye, Bw. Deus Musiba mkazi wa Buseresere ameeleza kuwa kwa kipindi kirefu barabara hiyo ilikuwa kikwazo kwa wananchi hasa kuzifikia huduma za kijamii ambapo wanafunzi walikuwa hawawezi kwenda shule kipindi cha masika lakini kwa sasa njia inapitika katika kipindi chote cha mwaka.
Kwaupande wake, Bi. Yustina Robert mkazi wa Buseresere ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kuondoa vikwazo katika barabara na kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi.
"Kwasasa wanafunzi wanaenda shule kwa urahisi hata sisi tunafaya kazi zetu bila kikwazo cha barabara tofauti na hapo awali", amesema Bi. Yustina.




No comments:
Post a Comment