WAZIRI MHAGAMA ALIOMBA BUNGE KUIDHINISHA TRILIONI 1.6 KWA AJILI YA SEKTA YA AFYA 2025/26 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 2, 2025

WAZIRI MHAGAMA ALIOMBA BUNGE KUIDHINISHA TRILIONI 1.6 KWA AJILI YA SEKTA YA AFYA 2025/26





Na WAF - Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewasilisha Bungeni makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya Shilingi Trilioni 1.68 kwa ajili ya kutumika kutekeleza vipaumbele na afua mbalimbali kwenye mwaka wa fedha 2025/26.

Waziri Mhagama amewasilisha bajeti hiyo, Bungeni jijini Dodoma Juni, 02, 2025 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Waziri Mhagama amesema Wizara ya Afya itaimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya milipuko, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, magonjwa yasiyoambukiza na huduma za lishe kwa kutekeleza afua mbalimbali.

Waziri Mhagama ameliambia Bunge kuwa suala la upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi taifa kwa kutekeleza afua ikiwa ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA ikiwepo akili mnemba (Artificial Intelligence) pamoja na kuunganisha mifumo iweze kusomana.

Waziri Mhagama ameongeza kuwa katika kipindi kijacho watajielekeza kwenye kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwepo kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya Sera za Kimataifa na ufadhili wa Sekta ya Afya.

"Tutaimaridha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kutekeleza afua ikijumuisha ununuzi na usambazaji wa dawa muhimu za uzazi salama pamoja na dawa za uzazi wa mpango, dawa kinga za minyoo, dawa za kuongeza damu, dawa za malaria, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi," amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama ameongeza kuwa bajeti hiyo imelenga upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi kwa kutekeleza afua kama vile kutoa ufadhili wa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa utaratibu wa seti kwa wataalam wa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi na kufadhili mafunzo ya kada za kati za kimkakati.

Kupitia fedha hizo trilion 1.6 Wizara itaimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuimarisha tiba utalii nchini kwa kutekeleza afua kwa kuendelea kutoa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa, Hospitali maalum, Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na kuanzisha na kuimarisha huduma mpya kulingana na mahitaji.

Eneo lingine litakalotiliwa mkazo ni kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa kutekeleza afua zinazojuisha kuuongeza Hospitali zinazotoa huduma jumuishi za Tiba Asili kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa 14 hadi 21.

Waziri Mhagama amefafanua kwamba ili kuitekeleza Bajeti ya mwaka ujao watahakikisha wanaimarisha upatikanaji wa huduma za tiba dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko kwa kuimarisha uzalishaji wa viuadudu katika viwanda vya ndani.

No comments:

Post a Comment