
Na Okuly Julius, DODOMA
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amewataka Watanzania kuendelea kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji na nishati ya umeme, ambayo ni mihimili muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma alipotembelea mabanda ya maonesho kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika kitaifa Juni 5 mwaka huu, Waziri Aweso alisema mabadiliko ya sera ya mazingira yaliyofanywa na serikali yanalenga kuendana na matakwa ya kimataifa.
Ameeleza kuwa mabadiliko hayo yamefungua fursa kwa serikali kushirikiana na wadau mbalimbali katika kulinda mazingira, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na yenye ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Mhe. Aweso aliwahimiza wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa ni msingi wa upatikanaji wa chakula na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Maria Holela, Afisa Usimamizi wa Mazingira kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), alisema bado kuna changamoto kubwa katika utunzaji wa miundombinu ya maji safi na maji taka, kutokana na wananchi kuendelea kutupa taka ngumu kwenye mifumo hiyo.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti Matumizi ya Plastiki.”

No comments:
Post a Comment