Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema matokeo ya Utafiti wa Ukatili dhidi ya Watoto na Vijana wa mwaka 2024 yanaonesha Ukatili umepungua ukilinganisha na Utafiti kama huo uliofanywa Mwaka 2009.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akitangaza matokeo ya utafiti huo Juni 9, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Gwajima amesema, utafiti huo unaonesha kupungua kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa kike ambapo, ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11, Ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 76 hadi asilimia 24 na Ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 25 hadi asilimia 22.
Aidha, kwa watoto wa kiume, Ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia 5, Ukatili wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi asilimia 21 na Ukatili wa kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.
"Naomba mfahamu kuwa, huu ni utafiti wa Pili wa kitaifa ambao umefanyika baada ya miaka 15 tangu utafiti ule wa kwanza wa mwaka 2009. Matokeo ya utafiti yanaonesha ukatili umeshuka kwa kiwango kikubwa ukilinganisha utafiti wa 2009 na huu wa 2024" amesema Dkt. Gwajima
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum itafanya tathmini, mapitio na maboresho ya Sera na Sheria zilizopo, sambamba na uimarishaji wa programu za kisekta za kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya makundi yote kwa kufanya uchambuzi wa afua zilizoainishwa katika MTAKUWWA wa Pili na kulinganisha na matokeo ya utafiti huu wa pili na hili litasaidia katika kuongeza bajeti na rasilimali watu ili kuzuia ukatili dhidi ya makundi yote na kuboresha huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili.
"Ninaomba kusisitiza kuwa, matokeo haya ya utafiti huu yatawezesha Serikali na Wadau kuboresha na kuandaa Mipango, Programu na Mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili nchini itakayoimarisha Ulinzi na Usalama wa Watoto na Vijana kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na cha baadae." amesisitiza Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima amesema, suala la ukatili dhidi ya watoto na vijana ni la ukiukaji wa haki za binadamu na pia linaleta changamoto kubwa za afya katika jamii na kubadilisha maisha ya watu wanaopitia ukatili.
Ameongeza kwamba, ukatili huleta athari za muda mrefu za kiafya ikiwa ni pamoja na matatizo ya afya akili, mawazo ya kujiua, tabia hatarishi za ngono, uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya zinaa ikiwemo VVU, matumizi ya dawa za kulevya. Pia ukatili hupunguza fursa mbalimbali za kimaendeleo na kuongeza umaskini katika jamii.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Amina Msengwa amesema, utafiti huo ni wa Kitaifa ambapo umefanywa katika mikoa 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia sampuli wakilishi ya Kitaifa hivyo, Takwimu hizo ni bora na zinafaa katika kuweka mipango mikakati na Programu na kufanya tathmini ya kuwalinda Watoto na Vijana dhidi ya Ukatili.
No comments:
Post a Comment