
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini nchini kuendelea kuihimiza jamii kuzingatia msingi ya maadili na kuepuka mienendo iliyo kinyume na tamaduni, mila na desturi ya Mtanzania
Amesema kuwa moja ya eneo ambalo viongozi hao wanapaswa kukemea ni kuhusu matumizi, biashara na usambazaji wa dawa za kulevya kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kunusuru maisha ya Watanzania hususan vijana.

Amesema hayo leo (Jumapili, Julai 13, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kumweka wakfu na kumuingiza kazini Askofu Mteule Dkt. Daniel Henry Mono wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
“Tuendelee kupambana vikali na matumizi ya dawa za kulevya sababu athari yake ni kubwa hasa kwa vijana wetu, vijana ni kundi tegemewa, matumizi ya dawa za kulevya yanaharibu uelewa na afya za vijana wetu”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuweka sheria kali pamoja na kuimarisha ukaguzi wa kubaini uingizaji wa dawa za kulevya nchini. “Tupo imara usikubali kushiriki katika biashara hii”.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameyapongeza madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuihudumia jamii ya Watanzania.

“Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini katika kufanikisha masuala mbalimbali yanayounganisha Taifa letu ikiwemo Agenda za kitaifa, kuimarisha masuala ya maadili na kujenga jamii inayozingatia misingi ya kudumisha upendo, amani na utulivu”
Ameongeza kuwa madhehebu hayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kutoa huduma za afya, elimu, malezi ya vijana, utunzaji wa mazingira pamoja na huduma kwa makundi maalum yenye uhitaji ikiwa ni kuinga mkono Serikali katika kutoa huduma.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali wakati wote itaendelea kufanya kazi na kushirikiana na madhehebu ya dini nchini kwa ajili ya manufaa ya watanzania wote.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia itaendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuimarisha ustawi wa wananchi katika nyanja zote za utoaji huduma pamoja na kusimamia uwepo wa Amani na Utulivu katika jamii.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 488 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya nia nne kuanzia Mailisita, Kiboriloni hadi Holili.
Mheshimiwa Majaliwa amepongeza Baba Askofu Mteule Dkt. Mono kwa kupewa nafasi ya kuiongoza Dayosisi ya Mwanga ambapo amesema uteuzi wake ni ishara kuwa amekidhi vigezo na kustahili kupewa daraja hili kubwa katika jamii.
“Ninakupongeza sana kwa kuwa umethibitika mbele ya Mungu na wanadamu, nafasi ya Askofu ni kubwa kwenye kanisa kwa kuwa askofu ni msimamizi wa kanisa. Kwa maneno mengine wewe ndiye kiongozi wa kiroho wa washarika wote wa Mwanga, hili ni jukumu kubwa sana ambalo unapaswa kulitekeleza kwa hekima kuu”.
Naye Askofu Mteule Dkt. Daniel Henry Mono ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuliombea Taifa hasa katika kipindi cha kuendelea uchaguzi mkuu utakaofanyika Mwezi Oktoba 2025 ili haki na amani viweze kudumua na mapenzi ya Mungu yaweze kutimia kwa kupata viongozi watakaoongoza kwa maslahi ya Taifa zima.
Ameongeza kuwa Dayosisi hiyo itaendelea kushirkiana na Serikali kama mdau mkubwa na mshirika wa karibu wa kanisa bila kuathiri misingi ya imani na kanisa.






No comments:
Post a Comment