
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) leo tarehe 22 Julai, 2025 wamesaini mkataba wenye lengo la kujenga kiwanda kipya cha kuzalisha nishati mbadala (Mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes) mkoani Geita ambapo mkataba huo una thamani ya shilingi bilioni 4.5.
Katika hafla iliyofanyika katika Ofisi ndogo ya REA, Jijini, Dar es Salaam, REA itatoa jumla ya shilingi bilioni tatu na STAMICO itatoa shilingi bilioni 1.5; kwa mchanganuo huo, REA itagharamia ununuzi wa mtambo wakati STAMICO italipia upatikanaji wa kiwanja, ujenzi wa jengo la kiwanda na gharama za ufungaji wa mitambo.
Mkataba huo umesainiwa na Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu wa REA pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse.
Mkataba huo utaifanya STAMICO kuwa na viwanda vikubwa vitano vya kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes; viwanda vingine ambavyo vinaendelea na uzalishaji wa mkaa mbadala vipo wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani, Kiwira mkoani Songwe, na viwanda vingine viwili vipo mkoani Dodoma na Tabora ambapo vipo kwenye hatua za mwisho za ukamilishwaji kabla kuanza uzalishaji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi, Hassan Saidy, amesema kuwa Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia unafikia asilimia 80 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2034.
“Katika kufanikisha lengo hilo, Wakala unatekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo uwezeshaji katika kuongeza uzalishaji na usambazaji ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa Watu wa vijijini.”
“Utiaji wa saini wa Mkataba huo kati ya REA na STAMICO ni moja wapo ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wakala ili kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa kuona namna ya kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nishati safi kwa Wananchi ili waondokane na matumizi ya nishati zisizo safi na salama”. Amesema Mhandisi, Hassan Saidy, Mkurugenzi Mkuu REA.
“Ni matumaini yetu kuwa Mkataba huu utaende kuongeza kasi ya upatikaji wa mkaa mbadala na kwa bei nafuu ikiwa ni mojawapo ya lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia. Tunatambua kuwa utunzaji wa mtambo huu ni muhimu sana ili huduma iliyokusudiwa iendelee kutolewa kwa wakati bila kuathili uchumi wa Wananchi, afya na pamoja na mazingira kwa ujumla”. Amekaririwa, Mhandisi, Hassan Saidy.
Mhandisi, Saidy ameongeza kuwa Wakala unaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Mkakati wa Nishati safi ya kupikia unatimiza malengo yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji na usambazaji wa mkaa mbadala, Wakala unaendelea kutekeleza Miradi mbalimbali ikiwemo usambazi wa majiko banifu, usambazaji wa majiko ya umeme, usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia majumbani (LPG ya kilo 6 na 15); usambazaji wa gesi asilia katika mkoa wa Lindi na Pwani pamoja na ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma.
Kwa upande wake, Dkt. Venance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO ameishukuru Serikali kupitia REA kwa mchango huu ambao utasaidia Shirika hilo kutimiza ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wote wanaachana na nishati isiyo safi na salama ya kupikia ifikapo mwaka 2034 na hivyo kuunga mkono juhudi za Serikali za kutunza mazingira.
“Hii ajenda ya matumizi ya nishati safi ambayo kinara wake ni Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kumkomboa Mwanamke ili aachane na nishati isiyo safi na salama. STAMICO tumejipanga kutekeleza maono haya ya Kiongozi wetu”, amesema Dkt. Mwasse.
Ameongeza kuwa nishati ya Rafiki Briquettes kwa sasa inatumiwa na Jeshi la Magereza ambapo Magereza yote 129 nchini kote yanatumia nishati hii kama aina mojawapo ya nishati ya kupikia, vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Taasisi nyingine ni pamoja na vyuo mbalimbali vya mafunzo, shule za msingi na sekondari, hoteli, migahawa, na sehemu wanazochoma nyama na chipsi.
Dkt. Mwasse amesisitiza kuwa STAMICO itaendelea kutunza mitambo hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa Wananchi.





No comments:
Post a Comment