
Mwakilishi wa Mbolea za Ruzuku Mkoa wa Dar es Salaam, Claudia Morandi, akitoa elimu ya Mbolea kwa mwanachi aliyembelea Banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania(TFRA) katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara( SABASABA) jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Julai, 2025.

Mtaalamu wa Maabara wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania(TFRA), Oscar Comred akitoa elimu ya mbolea kwa mwananchi katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 1 Julai,2025.


Wakulima na wafanyabiashara wa mbolea nchini wamehimizwa kutembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo katika banda hilo, Mwakilishi wa Mbolea za Ruzuku wa Mkoa wa Dar es Salaam, Claudia Morandi, amesema, utekelezaji wa mpango wa ruzuku za mbolea umelenga kumpunguzia gharama za uzalishaji mkulima na kumwezesha kupata mbolea kwa bei nafuu kupitia utaratibu rasmi wa kutumia namba ya mkulima.
Amesema pamoja na kutoa elimu ya matumizi na majukumu na fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye tasnia ya mbolea, Mamlaka itatoa huduma ya kuwasajili na kuhuisha taarifa za wakulima kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku.
“Mkulima anayetaka kusajiliwa au kuhuisha taarifa zake anafike na kitambulisho cha NIDA au cha mpiga kura.
"Baada ya usajili, atapewa namba ya utambulisho ya mkulima, ambayo utaitumia kununua mbolea pamojq na mbegu kwa mawakala waliothibitishwa na TFRA na Wakala wa Mbegu Tanzania zilizopo kwenye mpango wa ruzuku. Morandi amefafanua.
Morand, ameongeza kuwa, wakulima watakaotembelea banda hilo watapatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea, ikiwa ni hatua ya kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao, sambamba na kulinda afya na mazingira wanayofanyia shughuli zao.
Kwa upande mwingine, Mtaalamu wa Maabara kutoka TFRA, Oscar Comred, ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda hilo ili kujifunza kuhusu namna TFRA inavyodhibiti ubora wa mbolea kupitia uchambuzi wa virutubishi unaofanywa na Maabara ya Mbolea nchini.
“Maabara yetu hupokea na kuchunguza sampuli za mbolea kutoka kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaohitaji kusajili mbolea, wakulima, wanafunzi, Taasisi za utafiti ambapo Mbolea hizo hupimwa ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kitaifa na vya kimataifa kwa matumizi ya kilimo chenye tija.
Comred ameongeza kuwa, Maabara pia hufanya uchambuzi kwa sampuli kwa ajili ya ukaguzi ikiwemo mbolea zilizopo sokoni ili kujiridhisha endapo mbolea ni ile iliyopewa kibali cha kuingizwa nchini.
Maafisa wa TFRA wanaendelea kutoa huduma na elimu katika banda hilo hadi kilele cha maonesho hayo tarehe 13 Julai, 2025 huku wakulima na wananchi kwa ujumla wakihimizwa kujitokeza kwa wingi kuongeza uelewa wao kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa maendeleo ya kiuchumi.
No comments:
Post a Comment