MHE. CHUMI ATEMBELEA MAONESHO YA NANENANE 2025, ATOA WITO WA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUINUA KILIMO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 7, 2025

MHE. CHUMI ATEMBELEA MAONESHO YA NANENANE 2025, ATOA WITO WA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUINUA KILIMO


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.), kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ametembelea Maonesho ya ya Kilimo (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda ya washiriki, Mhe. Chumi amesema ameridhishwa na ubunifu, teknolojia bunifu na ushiriki mpana wa wadau kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo wajasiriamali, taasisi za utafiti, mashirika ya kimataifa na wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

“Maonesho haya ni jukwaa muhimu sana siyo tu kwa kukuza sekta ya kilimo, bali pia kuimarisha diplomasia ya uchumi kupitia uhamasishaji wa bidhaa na teknolojia bora za Kitanzania kupata masoko ya kimataifa,” alisema Mhe. Chumi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia maonesho hayo kama fursa ya kubadilishana maarifa na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa ufanisi na tija zaidi.

Katika mazungumzo na baadhi ya washiriki, wamejadili changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji, ikiwemo ukosefu wa mitaji, ukosefu wa dhamana za kiuchumi, masoko ya uhakika, pamoja na hitaji la uwekezaji wa Serikali katika sekta ya kilimo.

Mhe. Chumi amesisitiza kuwa majadiliano hayo yanaendana na mwelekeo wa Serikali wa kufikia maendeleo ya uchumi wa viwanda, ustawi wa wananchi, na kujenga jamii yenye uwezo wa kuzalisha kwa tija kupitia sekta za uzalishaji mali.

Maonesho ya Nanenane hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe mosi hadi nane Agosti, yakikutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali zinazohusiana na kilimo, mifugo, uvuvi na maliasili. 

Kaulimbiu ya maonesho hayo kwa mwaka 2025 inasisitiza umuhimu wa uongozi bora katika maendeleo, ikisema “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025.”


No comments:

Post a Comment