WATUMIAJI WA BARABARA YA CHAMWINO - DABALO - ITISO WAPATA SULUHISHO LA KUDUMU LA DARAJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, August 22, 2025

WATUMIAJI WA BARABARA YA CHAMWINO - DABALO - ITISO WAPATA SULUHISHO LA KUDUMU LA DARAJA



Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma Mhandisi Zuhura Amani, ameleeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa Daraja la mita 60 na upana wa mita 11.6, lililopo eneo la Nzali - Chilonwa, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma ambalo litakuwa ni suluhisho la kudumu kwa wananchi wa Wilaya hiyo.


Ameeeleza Ujenzi wa Daraja hilo upo katika barabara inayotoka Chamwino kuelekea Dabalo hadi Itiso ambapo ni barabara muhimu ya kiuchumi kwa wananchi wa Dodoma ambapo hadi hivi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 62.8.




Mhandisi Zuhura ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja hilo utakuwa mkombozi kwa wananchi kwa kuwa upana wake utakuwa na uwezo wa kutosheleza magari kupishana na njia ya watembea kwa miguu sambamba na uwekwaji wa taa kwa ajili ya ulinzi na usalama wa wasafiri na wasafirishaji.

Ameongeza kuwa ujenzi wa Daraja hilo ni mojawapo ya miradi ya dharura inayoendelea kutekelezwa kutokana na mvua za El- Nino zilizonyesha kuanzia mwezi Novemba 2023 hadi Mei 2024, na kuleta madhara ya uharibifu wa miundombinu ya madaraja katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.

“Daraja la Nzali - Chilono ni miongoni mwa maeneo yaliyopata athari za mvua hizo, eneo hili lilikuwa na Daraja dogo hivyo mvua zinaponyesha nyingi kunakuwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na eneo hilo kupita maji mengi na hivyo kuleta adha kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo", ameeleza Mhandisi Zuhura.

Aidha, Mhandisi Zuhura amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi CHICO kwa gharama ya Shilingi Bilioni 14.5 na kusimamiwa Kitengo cha TECU kutoka TANROADS ambapo mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2025.

Halikadhalika, Mhandisi Zuhura amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka TECU Mhandisi Leornard Mwambene ameeleza kuwa mradi huo umeweza kutoa ajira kwa wananchi wazawa 106 hadi sasa na kukamilika kwa daraja hilo utachochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Naye, Mkazi wa Nzali Bw. Leornard Mwambene ameeleza changamoto wanayoipata kipindi cha masika ambapo wananchi hutumia saa 2 hadi 3 kupita katika eneo hilo ili kusubiri maji yapungue na ameishukuru Serikali kwa kuwatafutia suluhisho la kudumu kwa kujenda daraja kubwa na litaloruhusu vyombo vya moto kupishana kwa urahisi.





No comments:

Post a Comment