DKT. BITEKO ASEMA KUPIGA KURA NI UWEKEZAJI WA MAISHA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 19, 2025

DKT. BITEKO ASEMA KUPIGA KURA NI UWEKEZAJI WA MAISHA


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amewaasa wananchi kushiriki katika zoezi la upigaji kura Oktoba 29 ili kuchagua viongozi watakaoweza kutimiza matarajio yao ya kuwaletea maendeleo.

Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 19, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Lyambamgongo wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

“ Uchaguzi ni uwekezaji wa maisha, kupiga kura na kuchagua viongozi inakupa uhalali wa kudai maendeleo kutoka kwa wale uliowachagua. Mimi huwa nashangaa mtu hapigi kura wala haudhurii vikao vya maendeleo lakini anakuwa wa kwanza kulalamika,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema wapiga kura wa Kata hiyo 4,600 waliojiandikisha wajitokeze kupiga kura na kuichagua CCM ili katika kipindi cha miaka mitano ijayo iwaletee maendeleo.

Ametaja baadhi ya mikakati ya CCM katika Kata hiyo kuwa ni kuwaletea gari ya wagonjwa pamoja na kufikisha umeme katika vitongoji saba ambavyo havijafikiwa na umeme.

Fauka ya hayo, amewaeleza wananchi hao kuwa katika uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwaruhusu wananchi wa Bukombe kuchimba madini katika Pori la Kigosi ili wapate fursa ya kujipatia kipato.

Pia, amesema Wilaya ya Bukombe haikuwa na stendi, soko la kisasa wala jengo la halmashauri hata hivyo Dkt. Samia ametoa fedha kwa ajili wa utekelezaji wa miradi hiyo hivyo wamchague kwa kumpa kura nyingi Oktoba 29.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa wananchi kutogawanyika kwa sababu yoyote ile hususan wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya Lyambamgongo, Boniface Shitobero amemshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara, zahanati mbili, madarasa na vifaa vya maabara katika shule za sekondari.

“ Kuna shule shikizi ambayo ametuletea fedha kwa ajili ya kujenga madarasa, kila kijiji kina umeme,” amesema Shitobero.

Aidha, amesema CCM ikipewa ridhaa ya kuongoza kwa miaka mitano ijayo itatekeleza miradi mipya kama shule na hospitali.

No comments:

Post a Comment