MSAADA WA KISHERIA KUTOLEWA KATIKA MAGEREZA 18 KANDA YA ZIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 19, 2025

MSAADA WA KISHERIA KUTOLEWA KATIKA MAGEREZA 18 KANDA YA ZIWA


Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza Tanzania inatarajia kutoa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Magereza 18 katika Kanda ya Ziwa katika mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga.

Akizungumza leo, Septemba 19, 2025 mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam watakaotoa Huduma za Msaada wa Kisheria katika Magereza hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi alisema kuwa huduma ya Msaada wa Kisheria inatolewa Magerezani na maeneo ya Vizuizini ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 iliyofanyiwa maboresho 2023.

“Sheria ya Msaada wa Kisheria inatuelekeza kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo na wale walio vizuizini, tumetekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia nchi nzima lakini hatukuweza kuwafikia mahabusu na wafungwa, hivyo tumeona ni vyema kuwafikia na kuwapa huduma za Msaada wa Kisheria kama sheria inavyoelekeza” alisema Msambazi.

Akizungumza wakati wa Mfunzo hayo Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Haruna Matata alisema kuwa lengo kubwa ni kutoa msaada wa kisheria katika maeneo ya Vizuizini na Magerezani ili kusaidia kupunguza msongamano katika maeneo hayo, pamoja na kutekeleza takwa la kikatiba na kisheria linaloagiza mtu yeyote asiyekuwa na uwezo kupewa Msaada wa Kisheria.

Matata alieleza kuwa utekelezaji wa zoezi hilo utaanza tarehe 22 Septemba, 2025 ambapo huduma mbalimbali za kisheria zitatolewa ikiwemo elimu, uandaaji wa nyaraka za kisheria kama vile nyaraka za rufaa, kuwasaidia mahabusu kufahamu mienendo ya mashauri yao pamoja na msaada wa uwakilishi mahakamani.

Kwa upande wake SSP Demetrius Masala, Mratibu wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Jeshi la Magareza, amesema kuwa utekelezaji wa zoezi hili la utoaji Msaada wa Kisheria katika Magereza utasadia kusikilizwa kwa kesi nyingi na kupatiwa ufumbuzi kwa muda mfupi sambamba na kuwasaidia mahabusu waliokosa haki kupata haki zao.

“Katika Magereza zetu, watu wengi walioko huku hawajui kusoma na kuandika, hivyo kwa Elimu na Msaada wa Kisheria unaoenda kutolewa wengi watasaidika, wanaohitaji kuandaliwa maombi ya dhamana, rufaa na nyaraka mbalimbali watapata pia” alisema










No comments:

Post a Comment