DKT. SAMIA AAHIDI HUDUMA BORA ZA KIJAMII NANYUMBU MKOANI MTWARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 23, 2025

DKT. SAMIA AAHIDI HUDUMA BORA ZA KIJAMII NANYUMBU MKOANI MTWARA


Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza dhamira ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kijamii na kiuchumi wilayani Nanyumbu, mkoani Mtwara.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni leo Septemba 23, 2025 kwenye Viwanja vya Stendi ya Nanyumbu Dkt. Samia amesema miradi inayotekelezwa na kuahidiwa inajikita kwenye sekta za afya, elimu, maji, barabara na biashara, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wananchi na kuharakisha maendeleo ya taifa.

Katika sekta ya afya, Dkt. Samia amesema wamejipanga kujenga na kuboresha miundombinu ikiwemo uzio wa Hospitali ya Mangaka, ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika Kata za Nandete, Sengenya na Napacho, pamoja na zahanati 14 vijijini. Vilevile, wodi tatu za wanaume, wanawake na watoto zitajengwa katika Kituo cha Afya Mikangaula sambamba na majengo ya mionzi matatu na jengo la upasuaji. “Tunataka kila mwananchi apate huduma bora za afya karibu na makazi yake,” amesema Dkt. Samia.

Kwa upande wa elimu, miradi mikubwa inahusisha ujenzi wa shule mpya tano za msingi na shule nne za sekondari, nyumba 31 za walimu, madarasa mapya na ukarabati wa shule kongwe. Aidha, serikali itajenga mabweni 10, maabara 10 na majengo ya utawala na TEHAMA katika shule mbalimbali. Ujenzi wa vyoo zaidi ya 400 umepangwa ili kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Katika sekta ya maji na mifugo, visima vitano vya umwagiliaji vitachimbwa ili kuongeza uzalishaji wa kilimo, huku mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mangaka ukitekelezwa. Vilevile, machinjio matatu ya kisasa yanajengwa ili kuimarisha sekta ya mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya nyama.

Sekta ya miundombinu na barabara pia haijaachwa nyuma, ambapo madaraja katika barabara kuu za Ndwika–Kalipinde, Mnanze–Nakole na Kazamoyo–Mokora yataimarishwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya wananchi.


No comments:

Post a Comment