
Baada ya kumaliza Mikutano ya Kampeni Unguja na Pemba, visiwani Zanzibar, Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea na mikutano ya Kampeni Mkoani Ruvuma, akitarajiwa leo Septemba 21, 2025 kuwa na mikutano Mbinga Mjini na Mbamba Bay Mkoani humo.
Jana Jumamosi, akiwa Chake Chake Pemba, Dkt. Samia pamoja na kuinadi Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na kuomba kura kwa wananchi, alisisitiza dhamira ya Chama chake katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania, akisema kaulimbiu yake ya Kazi na utu inanuia kuinua na kustawisha utu wa Mtanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata huduma bora za kijamii katika sekta za afya, maji, elimu pamoja na mahitaji mengine muhimu ya binadamu.

Alisisitiza pia umuhimu wa kulinda amani, akiwataka wananchi wa Pemba kutokubali kuchokozeka wakati huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa wakati huu wapo watu wanaochokoza wengine na kusisitiza kuwa Yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu hivyo vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimejipanga Kikamilifu kuhakikisha usalama na utulivu wakati wa uchaguzi Mkuu ili kutoa fursa kwa kila mwananchi kushiriki kupiga kura.
Katika Ilani ya Chama hicho kuelekea mwaka 2030, Dkt. Samia ameahidi kuendelea kuboresha uchumi, kuimarisha ustawi wa wananchi na kuhakikisha serikali itakayoundwa inaweka na kutekeleza mikakati thabiti ya kuinua hali ya maisha ya wananchi na kuboresha kipato cha kila Mtanzania.
CCM pia imeahidi kujenga majosho saba katika halmashauri za wilaya za Nyasa Dc, Tunduru, Songea Dc, Mbinga Dc na Madaba Dc, kujenga na kukarabati visima 3 katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na Songea Dc, kuimarisha huduma za chanjo, kinga na tiba za mifugo ili kuwezesha wafugaji kukabiliana na magonjwa na vifo, kuendelea kuboresha ufugaji wa mbuzi na kondoo pamoja na kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na mfumo baridi (Cold Chain) kwaajili ya kutunza chanjo za mifugo Mkoani Ruvuma.
Chama Cha Mapinduzi kupitia kwa Dkt. Samia kimeahidi pia kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya, kukamilisha ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa, kuongeza idadi ya majengo ya huduma za dharura katika hospitali za Wilaya za Mkoa wa Ruvuma kutoka 5 hadi 10, kufunga mashine ya kisasa ya MRI ili kuongeza uwezo wa kufanya uchunguzi wa kina na wa kisasa kwa wagonjwa, ukarabati katika miundombinu ya hospitali ya Mkoa ikiwemo jengo la mapumziko kwa ndugu wa wagonjwa pamoja na kuongeza idadi ya magari ya kubebea wagonjwa kutoka 26 hadi kufikia magari 36.
No comments:
Post a Comment