KAMISHNA WA UHIFADHI MSTAAFU MABULA MISUNGWI NYANDA AAGWA RASMI TAWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 20, 2025

KAMISHNA WA UHIFADHI MSTAAFU MABULA MISUNGWI NYANDA AAGWA RASMI TAWA


Na. Joyce Ndunguru, Morogoro.


Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imemuaga rasmi aliyekuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda baada ya kumaliza safari yake ya utumishi wa umma.

Akizungumza katika hafla hiyo ya Kijeshi iliyofanyika Septemba 19, 2025, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA yaliyopo Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Jen (Mstaafu) Hamis Semfuko alimpongeza Kamishna Nyanda kwa kuhitimisha safari yake ya utumishi na kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa kwanza wa TAWA aliyedumu kwa muda mrefu na kustaafu akiwa kwenye cheo hiko cha juu katika uongozi wa TAWA.

“Kwa namna ya kipekee ningependa kukupongeza na kukushukuru Kamishna Mstaafu Nyanda kwa utumishi wako katika tasnia hii ya uhifadhi na hususan ukiwa kama Kamishna wa TAWA,” alisema Mej. Jen (Mstaafu) Semfuko.

Sambamba na hilo, Semfuko aliongeza kuwa chini ya uongozi wa Kamishna Mstaafu Nyanda, TAWA imepata mafanikio mengi yakiwemo kuboresha maslahi ya watumishi, ujenzi wa miundombinu pamoja na kuongeza mapato ya Serikali, hususan baada ya uanzishwaji wa kuuza vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya kielektroniki pamoja na Uwekezaji Mahiri katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA.

“Mambo mengi ya kuijenga TAWA ikiwemo kubadilisha mifumo, kuboresha maslahi ya watumishi na mambo mengine yamefanywa chini ya uongozi wa Kamishna Nyanda, yeye akisaidiana na viongozi wengine ndio wameijenga TAWA kuwa hivi ilivyo sasa,” alisema Mej. Jen ( Mstaafu) Semfuko.

Kadhalika, Semfuko aliongeza kuwa Kamishna Nyanda, ameleta mabadiliko mengi ikiwemo kuongeza uadilifu na kuifanya TAWA kuwa imara zaidi.

“Umefanya kazi kubwa sana katika kujenga stability ndani ya TAWA, umeiacha TAWA ikiwa tulivu, imara na yenye nguvu zaidi,” alisema Semfuko.

Kwa upande wake, akitoa salamu za shukrani Kamishna wa Uhifadhi Mstaafu Mabula Misungwi Nyanda aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA kwa kutoa maono na miongozo iliyoweza kuifikisha TAWA ilipo sasa. Aidha, aliishukuru Menejimenti ya TAWA na watumishi wote kwa kuitekeleza miongozo hiyo iliyoleta mafanikio mengi katika Taasisi.

“Menejimenti na watumishi wa TAWA nyie ndio mliofanya mafanikio haya kuwa kweli, uaminifu wenu, weledi, juhudi na moyo wa uzalendo mlionyesha katika kulinda rasilimali za wanyamapori ni wa kupongezwa sana,”alisema Kamishna Mstaafu Nyanda.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Ndugu. Bernard Mercelline alimpongeza Kamishna Mstaafu Nyanda kwa kumaliza utumishi wake, Aidha, aliongeza kuwa kwa kupitia majukumu aliyoyatekeleza ameifanya TAWA ijulikane zaidi ya ilivyokuwa.

“Kwa niaba ya Wizara nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi njema uliyoufanya na nikushukuru kwa kazi nzuri,” alisema Mercelline.

Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA , Mlage Kabange alimshukuru Kamishna Mstaafu Nyanda kwa kuweka misingi imara na alisisitiza kuwa Menejimenti itaendelea kuyaenzi na kuyasimamia ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Taasisi yanafikiwa kwa viwango vya juu.

Hafla ya Kijeshi ya kumuaga Kamishna wa Uhifadhi Mstaafu Mabula Misungwi Nyanda iliambatana pia na tafrija fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Cate Hotel uliopo Mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment