MAGEREZA KATAVI WAPOKEA MAJIKO NA MITUNGI YA GESI KUTOKA REA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 27, 2025

MAGEREZA KATAVI WAPOKEA MAJIKO NA MITUNGI YA GESI KUTOKA REA


Wakala wa Nishati Vijjini (REA) kwa kushirikiana na kampuni ya ORYX Tanzania Ltd, tarehe 26 Septemba, 2025 imeanza zoezi la usambazaji wa majiko ya gesi na mitungi yake kwa Watumishi wa Jeshi la Magereza mkoa wa Katavi.

Akikabidhi majiko hayo ya sahani mbili na mitungi yake ya ujazo wa kilo 15; Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhandisi, Ahmed Chinemba amesema lengo la ugawaji wa majiko hayo pamoja na mitungi yake ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kila Mtanzania na kuongeza kuwa afya za Watanzania pamoja na mazingira yao ni kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita; inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi, Chinemba amesema Serikali kupitia REA imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Wananchi wakiwemo Watumishi wa Magereza ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa Mwaka 2024/2034 ambao unasisitiza angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishari safi ya kupikia ifikapo 2034

Akipokea majiko hayo pamoja na mitungi yake, Mkuu wa Magereza ya mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP); Shija Fungwe amesema Mradi huu umekuja katika wakati sahihi kwa kuwa Watumishi wa Jeshi la Magereza walikuwa wakitumia nishati zisizo safi na salama na kuahidi watayatumia majiko hayo na hata baada ya mitungi ya kwanza kuisha.

“Kimsingi Sisi kama Watumishi, tulikuwa tunatumia kuni na mkaa ajili ya mapishi ambapo kwa kweli, tulikuwa tukikata miti kama chanzo cha nishati, jambo hilo si zuri kwa ustawi wa mazingira. Mradi huu utatusaidia sana, tutanunua mitungi mingine kwa kuwa, tutakuwa tumeona faida ya kutumia gesi” alisema Kamishna Shija.

Naye, Mhandisi, Mbengwa Kasumambuto ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, amesema Serikali kupitia REA imewezesha kufungwa kwa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye Magereza yote ya Tanzania Bara kwa mifumo tofauti, ikiwemo mifumo ya LPG; miondombinu ya bayogesi; usambazaji wa makaa ya mawe (Rafiki briquettes) pamoja usambazaji wa majiko banifu makubwa kwa ajili ya kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu.

“Hadi sasa Magereza yote yakiwemo Magereza ya Katavi (Gereza la Katavi Makao Makuu; Gereza la Kalila Nkulukulu na Gereza la Mahabusu Mpanda) yanatumia aina moja au mbili za nishati safi kwa ajili ya kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu” amesema Mhandisi, Kasomambuto.

REA kwa kushirikia na Magereza wamendelea kuwafikia Watumishi wa Jeshi hilo ambapo tarehe 26 Septemba, 2025 ilikuwa ni zamu ya mkoa wa Katavi, jumla ya majiko ya gesi na mitungi yake 217 imeanza kusambazwa mkoani humo ambapo usambazaji umezinduliwa rasmi katika Gereza la Mahabusu Mpanda, mkoani Katavi.








No comments:

Post a Comment