MAJALIWA ; CCM IMEJIPANGA KUENDELEA KULETA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 21, 2025

MAJALIWA ; CCM IMEJIPANGA KUENDELEA KULETA MAENDELEO


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimejipanga kuendelea kuleta maendeleo katika sekta zote nchini.

Amesema kuwa Chama hicho mara zote kimekuwa kikigusa maendeleo kwa watanzania katika sekta zote hivyo kukichagua katika uchaguzi wa mwezi Oktoba 2025 ni uamuzi wa kuchagua maendeleo.

Amesema hayo leo Jumapili (Septemba 21, 2025) alipozindua kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Kiwani, katika viwanja vya Kwareni, Pemba Zanzibar. Mgombea Uwakilishi wa Jimbo hilo ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

"Wote ni mashahidi, Pemba ya leo, Zanzibar ya leo ni tofauti na tulipotoka, hatua za kimaendeleo katika maeneo haya ni mkubwa na yanaonekana kila sekta imeguswa, Mimi pia ni shahidi, nilifungua kituo cha afya hapa na sasa ninaambiwa kinatumika na mnanufaika nacho".

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wazanzibar kuchagua wagombea Urais wa CCM kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar kwa kuwa wameonesha wanaweza kusimamia maendeleo katika maeneo yao.

"Rais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi ni madaktari wa maendeleo, hawa wote ni wasikivu waadilifu waaminifu na wapenda maendeleo wachagueni viongozi hawa ili wafanya kazi nanyi, hawa ni wapenda maendeleo namba moja, wanasikiliza kero na kuzifanyia kazi"

Kwa upande wake mgombea Uwakilishi wa Jimbo hilo, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amewaahidi wananchi wa Jimbo hilo kuwatumikia kwa uaminifu mkubwa na ndani ya miaka mitano atazitatua changamoto katika eneo hilo.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake, atahakikisha kila kijana anayetoka katika jimbo hilo na kwenda kusoma popote watamfuatilia ili kusimamia maendeleo yake na kumuwezesha kunufaika na jitihada zake.


No comments:

Post a Comment