WAZIRI MKUU MAJALIWA KUFUNGUA MAONESHO YA MADINI GEITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, September 21, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA KUFUNGUA MAONESHO YA MADINI GEITA



Na Mwandishi Wetu, Geita. 


Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita yanatarajiwa kuzinduliwa kesho na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, Manispaa ya Geita.

Akizungumza leo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Samwel Shoo, amesema Tume ya Madini inashiriki maonesho hayo kwa mara ya nane mfululizo na imeandaa huduma za elimu kwa wadau wote wa sekta ya madini watakaotembelea mabanda yake. Elimu hiyo itahusu teknolojia za kisasa za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

“Huu ni msimu muhimu unaowaunganisha wachimbaji, wachenjuaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa madini ili kubadilishana ujuzi na kujifunza mbinu mpya. Pia ni nafasi ya kuimarisha uhusiano wa sekta ya madini na sekta nyingine za kijamii na kiuchumi,” amesema Shoo.

Ameongeza kuwa ni fursa kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa pamoja na wawekezaji kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika katika sekta ya madini.

“Lipo Banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake, ikiwemo Tume ya Madini. Ni muhimu Watanzania wenye nia ya kuwekeza wakatembelea mabanda haya ili kupata elimu ya kina kuhusu mnyororo mzima wa sekta ya madini,” amesisitiza.

Maonesho hayo mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia Sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.”






No comments:

Post a Comment