TaFF YAJIFUNZA NCHINI UFINI NAMNA BORA YA KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA SEKTA YA MISITU TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 23, 2025

TaFF YAJIFUNZA NCHINI UFINI NAMNA BORA YA KUSHIRIKISHA SEKTA BINAFSI KATIKA KUENDELEZA SEKTA YA MISITU TANZANIA




Na Mwandishi Wetu


Wataalamu kutoka kutoka Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Idara ya Misitu na Nyuki na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) wamefanya ziara nchini Ufini kujifunza kuhusu namna bora ya kushirikisha sekta binafsi katika kuendeleza sekta ya misitu nchini. Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ubalozi wa Ufini nchini Tanzania ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii za kubadilishana uzoefu kati ya wataalam wa Tanzania na wale wa Ufini juu ya ushirikishwaji sahihi wa sekta binafsi katika uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali misitu.

Akizungumzia wakati wa ziara hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt Tuli S. Msuya alisema kuwa ziara hiyo itasaidia utekelezaji wa Mkakati wa TaFF wa Utafutaji Fedha (Fundraising Strategy) wenye lengo la kutanua wigo wa vyanzo vya mapato ili kuongeza uwezo wa TaFF kujiendesha iwapo vyanzo vya sasa vinavyotokana na maduhuli ya misitu havitakuwepo.

“Tumejifunza namna bora ya ushirikishwaji na uwezeshaji wa sekta binafsi katika mnyororo mzima wa shughuli za uhifadhi, uendelezaji na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu katika kuchangia ongezeko la kipato cha jamii na Uchumi wa nchi. Mafunzo hayo pia yanatoa fursa kwa TaFF kuanzisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa Ufini katika ushirikishwaji na uwezeshaji wa sekta binafsi nchini” Aliongeza Dkt. Msuya

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Misitu na Nyuki Bw. Seleboni J. Mushi, alisema kuwa mafunzo hayo yana faida kwa maendeleo ya misitu nchini kwa sababu eneo lenye misitu ni zaidi ya asilimia 40 ya ardhi ya Tanzania, lakini mchango wake katika pato la Taifa bado ni mdogo (takribani asilimia 4 tu). Hivyo, ni muhimu kuhamasisha sekta binafsi ili iongeze ushiriki katika mnyororo wa shughuli za misitu na kutumia teknolojia ambazo zinaongeza uzalishaji na matumizi sahihi ya mazao ya misitu. Aidha, sekta binafsi inaweza kuwekeza katika huduma za utalii na kuongeza pato la taifa na ajira kama inavyofanyika nchini Ufini ambapo idadi ya Watalii ni takribani watu milioni 8 kwa mwaka.

Washiriki wengine kutoka TaFF na Ofisi ya Msajili wa Hazina walisema kuwa ziara hiyo ya mafunzo itasaidia kuendeleza shughuli za uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali misitu nchini Tanzania kwa kuangalia utaratibu mzuri wa kuwezesha sekta binafsi ili zishiriki katika uwekezaji kwenye teknolojia zenye tija katika uvunaji na uchakataji wa mazao ya misitu nchini Tanzania.

Walioshiriki ziara hiyo ya mafunzo ni Bw. Seleboni J. Mushi, Mkurugenzi Msaidizi - Maendeleo ya Misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii; Dkt. Tuli S. Msuya, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TaFF; Dkt. John R. Mbwambo, Mkuu wa Kitengo cha Miradi na Mipango - TaFF; Bi. Emiliana M. Mallya, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu - TaFF, na Wenceslaus B. Myanjamu kutoka OTR.







No comments:

Post a Comment