Timu zachukuana kuchukua ubingwa wa jumla SHIMIWI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 11, 2025

Timu zachukuana kuchukua ubingwa wa jumla SHIMIWI



Na Mwandishi Wetu, Mwanza


Timu zinazoshiriki kwenye michezo ya 39 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) zimechuana vikali kwenye mchezo wa riadha kuwania ubingwa wa jumla, ambao unatokana na kupata medali nyingi katika mchezo wa riadha.

Kwa mujibu wa matokeo ya mchezo huo, timu za Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU), Mahakama, Mashtaka, Utumishi, Wizara ya Elimu na Wizara ya Uchukuzi zinachuana baada ya wanariadha wake kushika nafasi mojawapo kati ya tatu za juu katika mbio mbalimbali.

Katika michezo ya fainali iliyochezwa leo tarehe 11 Septemba, 2025 washindi wa mita 400 kwa wanawake ni Mastura Kaiza wa Wizara ya Uchukuzi, kafuatiwa na Happiness Dominic wa RAS Mara na Grace Mkunda wa TAKUKURU; wakati kwa wanaume ameshinda Pwele Jackson wa Elimu, akifuatiwa na Hassan Shaban wa Mashtaka na Edger Mtimba wa Mahakama.

Bingwa wa mbio za mita 100 wanawake ni Judith Malata wa Mashtaka, aliyefuatiwa na Furaha Kagoneka wa Ukaguzi na Leah Danda wa Mahakama; wakati kwa upande wa wanaume ameshinda Paul Tarimo wa TAKUKURU, aliyefuatiwa na Pwele Jackson wa Elimu na Dotto Zegeli wa Mashtaka.

Mwanariadha Justa Tibenderana wa Mahakama ameibuka mshindi wa mbio za mita 1500 kwa wanawake na kufuatiwa na Mary Paulo wa Wizara ya Katiba na Sheria, na Eudes Kamulali wa Ofisi ya Bunge; huku kwa wanaume ameshinda Paul Rema wa TAKUKURU, akifuatiwa na Joseph Kachalla wa Wizara ya Afya na Peter Mwaya wa Ofisi ya Rais Managementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katika fainali za mbio za mita 200 wanawake ameshinda Judith Malata wa Mashtaka, akifuatiwa na Mastrura Kaiza wa Wizara ya Uchukuzi na watatu Mwajabu Bwire wa Mahakama; wakati kwa wanaume kashinda Ramadhani Awadhi, aliyefuatiwa na Pwele wa Elimu na Julius Mwageni wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Fainali za mita 100 wachezaji watu wazima wanaume ameshinda Suleiman Juma wa Nishati, akifuatiwa kwa karibu na Charles Masanja wa RAS Mara na wa tatu ni Florence Prudence wa RAS Kagera; na katika mbio za kupokezana vijiti (relay) mita 100x4 kwa wanawake imeshinda timu ya Utumishi, wakafuatiwa na Mahakama na Wizara ya Maji; wakati kwa wanaume wameshika usukani TAKUKURU, wakafuatiwa na Utumishi na Mashtaka.







No comments:

Post a Comment