
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John C. Mbisso,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, kuelekea Mkutano wa Kwanza wa Tume unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 17 Oktoba 2025 jijini Dodoma.
NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2025/2026, unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 17 Oktoba 2025 jijini Dodoma, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) eneo la Njedengwa.
Mbisso ametoa taarifa hiyo leo Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema mkutano huo utakuwa ni fursa muhimu kwa Tume kupokea, kujadili na kutoa maamuzi juu ya rufaa na malalamiko mbalimbali yaliowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na maamuzi ya waajiri wao, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu.
"Tume ina wajibu wa kisheria kupokea hoja hizo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma (Sura ya 298, marejeo ya 2023) pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022,"
"Tume ya utumishi wa umma imepanga kujadili na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko mbalimbali zaidi ya mia moja yaliyowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka zao za nidhamu," amesema Mbisso
Mbisso pia ameongeza kuwa katika mkutano huo, warufani au warufaniwa walioomba watapewa nafasi kupiga hoja zao mbele ya Tume, kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu rufaa zao, kama vile inavyowekwa wazi kwenye Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma. Aidha, taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa robo ya tatu na robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 zitawekwa mbele ya wajumbe wa mkutano kwa majadiliano na utoaji wa mwelekeo.
Akizungumza juu ya umuhimu wa mkutano huo, Mbisso amesisitiza kwamba ni sehemu ya uwajibikaji wa Tume kuhakikisha utendaji kazi wa utumishi wa umma unafuatana na sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayoweka haki na uwazi kwa watumishi wote. Katika hafla nyingine, amefungua kikao kazi cha ndani cha Tume ambapo aliagiza mapitio ya miongozo ya ndani, akisisitiza kuwa Tume lazima iendelee kujiboresha ili kuendana na mahitaji ya wakati na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment