Imeelezwa kuwa, utendaji kazi wa Wizara ya Nishati kupitia Taasisi inazosisimamia umezidi kuimarika na kufikia asilimia 96.16 katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025.
Hayo yamefahamika wakati wa kikao cha Tano cha Tathmini ya utendaji kazi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa robo nne ya mwaka 2024/2025 kilichofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba.
Tathmini hiyo ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati imeonesha kuwa katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa Taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati umeimarika kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka asilimia 95 katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025.
Kufuatia tathmini hiyo, Mha. Mramba amewapongeza Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kuboresha utendaji kazi kupitia utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi hali inayoleta matokeo chanya katika Sekta ya Nishati.
“Tathmini hizi zinaakisi kile tunachokitekeleza kwani huduma zimeendelea kuboreshwa pamoja na kuimarika zaidi, sisi kama Wizara tumeendelea kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora kwa wananchi”.Ameeleza Mha. Mramba
Katika kikao hicho, Mha. Mramba amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati jambo ambalo limeleta ongezeko la kuimarika kwa utoaji huduma.
Aidha, kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, amesisitiza kutumia mitandao ya kijamii katika kuitangaza nishati hiyo hususani matumizi ya majiko yanayotumia umeme kidogo akieleza kuwa mitandao ya kijamii inanguvu kubwa ya kufikisha habari kwa watu wengi na kwa muda mfupi lengo likiwa ni kutimiza adhma ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka matumizi ya Nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Vilevile, amekipongeza Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Nishati kwa kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi huku akisisitiza kuwa Kitengo hicho kipewe ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Idara, Vitengo na Taasisi zinawasilisha taarifa za utendaji kazi kwa wakati ili kitengo hicho kiongeza ufanisi zaidi katika kazi ya tathmini na hivyo kuboresha utendaji kazi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amezipongeza Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na Idara na Vitengo vya Wizara ya Nishati kwa utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya kama ambavyo tathmini ya utendaji kazi ilivyoonesha kuwa ufanisi wa kazi umeendelea kuboreshwa na kuimarika zaidi.
Awali, Akiwasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji kazi kwa Wizara na Taasisi zake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Wizara ya Nishati, Bi. Anita Ishengoma alisema kuwa kutoka zoezi la tathmini lianze kufanyika, limeleta ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na mipango ya Wizara kwani utendaji kazi wa Taasisi umeongezeka.
Amesema kuwa Idara/Vitengo zilizofanya vizuri zaidi katika tathmini iliyofanyika katika Wizara ya Nishati kwa kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Idara ya Umeme na Nishati Jadidifu (nafasi ya kwanza), Kitengo cha Manunuzi -(Nafasi ya Pili) na - Kitengo cha Tehama ( Nafasi ya Tatu).
Aidha, Taasisi zilizofanya vizuri zaidi katika utendaji kazi kwa tathmini iliyofanyika katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) - nafasi ya kwanza), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) -nafasi ya Pili) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA)- nafasi ya Tatu).
Mikoa ya Kitanesco iliyofanya vizuri katika utendaji kazi kwa tathmini iliyofanyika katika kipindi cha robo nne ya mwaka 2024/2025 ni Manyara (nafasi ya kwanza), Kinondoni Kusini ( nafasi ya Pili) na Simiyu ( nafasi ya Tatu).
Ilielezwa kuwa utendaji kazi wa mikoa ya kitanesco kwa ujumla umeimarika kwani hamna mkoa ambao utendaji wake umekuwa chini ya asilimia 91.83.
Katika Kikao hicho pia Taasisi ziliweza kuwasilisha taarifa za utendaji kazi wake.
kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakurugenzi wa Vitengo Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara mbalimbali, Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake pamoja na Mameneja wa Kanda wa TANESCO.
No comments:
Post a Comment