
Na. Joyce Ndunguru, Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewakaribisha Sekta Binafsi kuwekeza katika maeneo ya Hifadhi Nchini, ikiwemo Hifadhi ya Swagaswaga ambayo ni kitovu cha utalii katika Jiji la Dodoma.
Dkt. Abbasi aliyasema hayo, Septemba 26,2025, alipofanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Swagaswaga iliyopo katika Mikoa ya Dodoma na Singida.
“Tumetenga maeneo ya uwekezaji katika hifadhi, hivyo tunawaalika sekta binafsi kwa ajili ya kusaidiana na sisi”, alisema Dkt. Abbasi.
Kadhalika, Dkt. Abbasi aliipongeza TAWA kwa ujenzi wa miundombinu ya awali katika Hifadhi ya Swagaswaga ikiwemo ujenzi wa hosteli kwa ajili ya watalii, ujenzi wa Ofisi, ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na ujenzi wa barabara na alisisitiza kuwa Wizara itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya utalii katika maeneo ya hifadhi.
Awali ,akimkaribisha Dkt. Abbasi, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yussuf Kabange alisema TAWA inaendelea na mikakati mbalimbali ya utangazaji na uboreshaji wa miundombinu katika Hifadhi ya Swagaswaga ili kuhakikisha Hifadhi hiyo inafikika kiurahisi zaidi na inaendelea kupokea wageni wengi zaidi.
Hifadhi ya Swagaswaga inapatikana takribani kilometa 140 kutoka Mkoa wa Dodoma na imesheheni vivutio mbalimbali wakiwemo wanyamapori kama vile Tembo, kudu, twiga na spishi mbalimbali za ndege.
Hifadhi hii pia imesheheni michoro ya miambani (Mapango yenye alama za kihistoria) kutoka katika jamii ya Wasandawe.






No comments:
Post a Comment