Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hatua kubwa za kimaendeleo zimepigwa Mkoani Rukwa katika sekta ya ujenzi wa miundombinu akiahidi pia kusimamia ujenzi wa barabara ya Kibaoni-Majimoto- Muze-Kiliamatundu ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Niwaambie kwamba hii ni barabara nitakayoisimamia kwa nguvu zote, nilipokuja kwenye Kampeni 2015 nilipangwa kwenda Muze, Mkuu wa Mkoa wa wakati ule akanisihi sana kwamba Mama usiende Muze kwa barabara kwani hakukuwa vizuri hata kidogo, ilibidi niruke kwa helkopta kwenda Muze na Ujumbe wangu wote ulienda kwa barabara, kurudi kila mtu jasho linamtoka, nawambia vipi wanasema hatari tupu. Yale yaliyotokea wakati ule sitaki yatokee tena, nitaisimamia kuhakikisha watu wanaoshuka kule Muze wawe na uhakika wa safari." Amekaririwa akisema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Sumbawanga Mjini kwenye Viwanja vya Kizitwe wakati wa Mkutano wake wa mwisho wa kampeni Mkoani humo leo Oktoba 19, 2025, akiahidi pia kuendeleza miundombinu mingine ya barabara katika Wilaya za Mkoa huo.
Ameahidi pia kusimamia ujenzi wa barabara ya Matai- Kasesya ya Kilomita 50 sambamba na ujenzi wa Kituo cha Mabasi ya Laela kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani humo.






No comments:
Post a Comment