Kesi Na. ECC. 9258/2026 inayowakabili watu watatu kwa tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya shilingi milioni 103 imeanza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kigoma mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Anna Kuhungu.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Kulwa Ryoba James, Gaudens John Ndolo na Pamhilius Gerald Gagwa ambao wanakabiliwa na makosa mbalimbali ikiwemo matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, ufujaji na ubadhilifu, kusaidia kutendeka kwa kosa pamoja na kughushi.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na waendesha mashtaka kutoka TAKUKURU, Bw. Augustino Lohay na Bw. James Nyarobi, umeieleza mahakama kuwa washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Julai na Agosti 2022.
Inadaiwa kuwa washitakiwa walitumia hati za malipo zenye thamani ya shilingi 103,000,000 mali ya Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Tanganyika Kigoma Mjini (LTBWB), kwa kuwasilisha taarifa za uongo za kuwalipa watumishi hewa wakati wa zoezi la utambuzi na ukaguzi wa vyanzo vya maji katika wilaya za Kibondo, Kakonko, Biharamulo na Ngara.
Hata hivyo, washitakiwa wote wamekana mashtaka hayo waliposomewa mahakamani.
Baada ya kusomewa masharti ya dhamana, washitakiwa walishindwa kuyatimiza na hivyo kupelekwa mahabusu hadi watakapokidhi masharti hayo.
Kesi hiyo imeahirishwa na itatajwa tena Mei 14, 2026.


No comments:
Post a Comment