
Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Mkuranga Mkoani Pwani na Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega amesema katika miaka minne na nusu ya Uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan takribani Shilingi Trilioni Moja na Bilioni mia saba zimetolewa katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar Es salaam.
Waziri Ulega amesema lengo la uwekezaji huo mkubwa uliofanywa na Dkt. Samia ni kuhakikisha Jiji la Dar Es Salaam linaondokana na changamoto ya foleni na msongamano mkubwa wa magari, suala linaloathiri shughuli za kiuchumi kutokana na wananchi wengi kutumia muda mwingi barabarani. Mhe. Ulega ametoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni Mkoani Dar Es salaam.
"Trilioni moja na Bilioni mia saba ni hela nyingi sana, umezielekeza katika mambo makubwa mawili; kuondoa msongamano Dar Es Salaam na kuwarahisishia Dar Es salaam waweze kusafiri kwa urahisi ili kutopoteza muda mwingi kwenye foleni na umekuwa ukihuzunika sana na hili tatizo la foleni na misongamano na ndiyo maana kwenye fedha hizo zipo fedha za kuondosha msongamano na nyingine kuondoa mafuriko hapa Dar Es Salaam na ndio maana tunasema Dkt. Samia wewe una utu kwasababu kila daraja, kina Kilomita unayoamuru ijengwe inanusuru utu wa Mtanzania." Amesisitiza Waziri Ulega.
Amesema kulingana na maelekezo ya Dkt. Samia, lengo lake ni kuhakikisha foleni zinaisha Mkoani humo pamoja na kuondoa adha ya mafuriko katika Jiji hilo, akisisitiza hitaji la kumuunga Mkono Dkt. Samia na kumuombea kwa Mwenyenzi Mungu ili aendelee kuwatumikia watanzania wote.
Aidha amezungumzia pia utatuzi wa changamoto ya mafuriko kwenye eneo la jangwani, Temeke Dar Es salaam akisema shilingi Bilioni 97 zimetolewa na serikali ya Awamu ya sita ili kujenga daraja la urefu wa Mita 400 katika eneo hilo akieleza kuwa Historia ya Tanzania, Afrika na dunia nzima itamkumbuka kwa hatua kubwa za kimaendeleo zilizopigwa katika sekta ya miundombinu nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment