
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi wananchi wa Mkoa wa Dar Es Salaam kuwa kuanzia Januari 2026, wananchi hao watashuhudia mapinduzi makubwa ya maboresho kwenye sekta ya usafiri kwa mabasi yaendayo kasi BRT.
Dkt. Samia ameahidi hayo leo Jumanne Oktoba 21, 2025 wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar Es Salaam kwenye viwanja vya Leaders Club kwenye muendelezo wa kampeni za uchaguzi Mkuu, akiahidi kusimamia kikamilifu maamuzi ya serikali ya kutoa huduma hiyo kwa sekta binafsi ili waendeshe usafiri huo wa mwendokasi.
Akizungumzia uwekezaji uliofanywa kwenye ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka, Dkt. Samia amesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali yake, jumla ya Kilomita 94.9 za barabara zimejengwa ambapo takribani Shilingi Trilioni 2.100 zimetumika katika ujenzi wake.
Akieleza kuhusu utekelezaji wa maazimio ya kukabidhi huduma hiyo kwa sekta binafsi, Dkt. Samia amesema tayari Kampuni ya EnG imeanza kazi hiyo kwa kuingiza mabasi 177, Mofat wakiwa na mabasi 255 huku pia Kampuni za Yglinks yenye mabasi 166 na Metrolinkcity yenye mabasi 334 zikitarajiwa kuanza kazi zake punde tu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara za mwendokasi kwenye maeneo mbalimbali Mkoani humo.
No comments:
Post a Comment