
Mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Ubungo Mkoani Dar Es Salaam ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jimbo la Ubungo limeongeza Mtandao wa barabara za lami kutoka Kilomita 32. 78 hadi kufikia Jumla ya Kilomita 78.98 suala lililowezesha huduma za usafiri na usafirishaji kuwa rahisi zaidi.
Prof. Kitila amebainisha hayo leo Jumanne Oktoba 21, 2025 wakati wa Kampeni za Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, akisema mpaka kufikia Disemba 2025 Wilaya ya Ubungo itakuwa imefikia lengo la kufikia asilimia 50 kutoka 46.8 ambazo zimefikiwa mpaka sasa Oktoba 2025.
Kitila amebainisha kuwa wamefikia hatua hiuo baada ya Dkt. Samia kuridhia na kutoa fedha za utekelezaji wa Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) kwa Wilaya za Ubungo na Kigamboni ambapo kwa Ubungo Pekee kupitia mradi huo jumla ya Kilomita 25.12 zimejengwa ikiwemo barabara 12 ndani ya Kata ya Sinza.
Barabara nyingine zilizojengwa kupitia mradi wa DMDP ni pamoja na barabara ya Manzese na Makurumla, barabara korofi ya Midizini- Tiptop Manzese, Barabara ya Makoka (Km4.04), Barabara ya Binti Kayenga Kata ya Mabibo, barabara ya Ubungo National Housing na barabara tatu za Kata ya Kimara sambamba na barabara ya Kimara- Bonyokwa- Kinyerezi.
"Barabara hii ya Kimara- Bonyokwa- Kinyerezi iliahidiwa mwaka 2010 na Dkt. Kikwete, Rais wa awamu ya nne ikaitwa Kikwete Highway lakini haikujengwa, ikaahidiwa mwaka 2015, mwaka 2020 haikuwezekana, Mwaka 2021 tulikulilia hatimae mwaka 2022 ukaidhinisha iingie kwenye bajeti ya mpango wa maendeleo na mwaka jana umeruhusu zikatoka fedha, Mkandarasi ameingia na sasa yupo kwenye barabara ya Kimara Bonyokwa."amesema Prof. Kitila.
Kulingana na Kitila, barabara hiyo inaunganisha Wilaya za Ubungo na Ilala pamoja na kuunganisha majimbo matatu ya Kibamba, Ubungo na Segerea, ikiwa na urefu wa Kilomita 8, ikitajwa kuwa Mkombozi wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa Wilaya hizo za Ubungo na Ilala Mkoani Dar Es Salaam.
No comments:
Post a Comment