Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI ambaye pia ni Mgombea wa nafasi ya Ubunge Jimbo la Rufiji Mkoani Pwani Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Jumla ya Kilomita 1600 za mtandao wa barabara za lami zimejengwa nchi nzima pamoja na kukarabati barabara za Changarawe za Kilomita 1300 nchi nzima.
Mchengerwa amebainisha hayo leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 wakati wa Kampeni za Mgombea Urais kwa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri Mkoani Pwani akisema Dkt. Samia pia amefanikiwa kuunganisha wakulima na Masoko kwa kujenga madaraja 5,000 chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA.
"Kimsingi hujajenga madaraja, umeuwanganisha wananchi wa Mashambani na wale walioko sokoni." Amesema Mhe. Mchengerwa.
Kwa Rufiji Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya awamu ya sita imejenga Daraja la Mbambe lililogharimu Shilingi Bilioni 27, daraja la Muhoro pamoja na Daraja la Bibi Titi Mohamed, akisema madaraja hayo yamesaidia kuondoa changamoto ya mafuriko na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji Mkoani humo.
Akimtaja Dkt. Samia kama Shujaa wa maendeleo ya Tanzania, Mchengerwa pia amemshukuru Dkt. Samia kwa kuamsha na kutekeleza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kusema mradi huo mbali ya kuwa ndoto ya Baba wa Taifa imeihakikishia Tanzania umeme wa uhakika na kuondoa tatizo la mgao.
No comments:
Post a Comment