
Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Songwe
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekabidhi pikipiki nane kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Songwe ili kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika leo tarehe 23 Oktoba, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoka halmashauri nne kati ya tano za Mkoa huo.
Akizungumza wakati wa kukabidhiano ya pikipiki hizo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Felister Mdemu, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma zaidi, akisema Serikali imewapatia nyenzo hizo muhimu ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika jamii.
“ Pikipiki hizi ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuwawezesha watumishi kufanya kazi zao kwa ufanisi. Tunatambua mchango mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kufikia wananchi na kuratibu shughuli za maendeleo, hasa katika maeneo ya vijijini,” amesema Mdemu.
Mdemu ameongeza kuwa lengo kuu la kugawa pikipiki hizo ni kutambua thamani ya mchango wa Maafisa hao katika jamii, sambamba na kurahisisha kazi za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, masuala ya ustawi wa jamii, na huduma kwa makundi maalum kama wanawake, vijana, wazee, na watu wenye ulemavu.
“Tunataka kuona matokeo chanya ya uwezeshaji huu, Pikipiki hizi ziwasaidie kufika mbali zaidi, kufuatilia miradi kwa karibu, na kuwahudumia wananchi ipasavyo. Serikali inatarajia kuona manaongeza uwajibikaji na ubunifu katika kazi zenu,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe John Mwaijulu aliishukuru Wizara kwa hatua hiyo, akisema kuwa uwezeshaji huo utasaidia kupunguza changamoto ya usafiri iliyokuwa inawakabili Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa muda mrefu, jambo lililokuwa likichelewesha utekelezaji wa baadhi ya majukumu yao.



No comments:
Post a Comment