
Songea, Ruvuma
Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuondoa vikwazo katika Barabara wilayani Songea kwa ujenzi wa daraja la Mto Lumecha na kufungua barabara ya kilomita 4 katika kata ya Mkongotema sambamba na ujenzi wa daraja la Mto Liweta iliyopo katika Kata ya Mpandangindo.
Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Bakari John, ameeleza kuwa hizo ni juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara zikilenga kuinua uchumi wa wakulima wa Wilaya ya Songea kupitia mradi wa RISE programu ya Uondoaji Vikwazo katika Barabara (bottleneck) iliyopo chini ya TARURA.
"Wananchi wa Mkongotema na Mpandangindo, ambao ni wakulima wa mazao ya biashara kama tangawizi, mahindi na parachichi, walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi sokoni".
“Kukosekana kwa miundombinu bora kulisababisha gharama za usafirishaji kuwa juu na kupunguza faida kwa wakulima. Ujenzi wa madaraja na barabara umeleta mabadiliko makubwa, na sasa wakulima wanaweza kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi”. Amefafanua
Aidha, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Awamu ya Sita, Wilaya ya Songea imefanikiwa kufungua barabara mpya zenye urefu wa kilomita 192 na kuongeza kuwa barabara hizo zimeelekezwa mashambani, hatua inayolenga kuchochea uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa mazao.
Mhandisi Bakari ameongeza kuwa madaraja makubwa 6 yenye urefu wa zaidi ya mita 25 yamejengwa, huku madaraja madogo zaidi ya kumi (10). “Miundombinu hii imekuwa mkombozi kwa wakulima na jamii kwa ujumla, ikirahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii”.
Hata hivyo Mhandisi Bakari amesisitiza umuhimu wa kutunza miundombinu hiyo kwa kuwa serikali inatumia fedha nyingi kuijenga. “Ni wajibu wetu kuilinda ili iweze kuwanufaisha vizazi vijavyo,” amesema.
Naye, Bw. Edsnon Lunji mkazi wa Madaba-Mkongotema amesema zamani hawakuwa na barabara bali kulikua na njia ya kutembea kwa miguu na magari yalikuwa yanazunguka umbali mrefu ambapo gharama yake ilikuwa ni kubwa sana, hivyo anaishukuru serikali kwa kuwachongea barabara na ujenzi wa daraja kwani kwa sasa itawarahisishia usafirishaji wa mazao.
Kwa upande wake Bw. Baitan Nyoni mkazi wa Mkongotema amesema barabara hiyo inakuwa ni ya mkato na ameishukuru serikali kwa kuwaona kwani sasa watasafirisha mazao yao kwa gharama nafuu na hata mara mbili kwa siku, amesema awali walikuwa wakitumia kivuko cha miti ambapo watu wengi walidumbukia mtoni na kuhatarisha maisha yao.




No comments:
Post a Comment