
Na Mwandishi Wetu,Mbeya
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kutumia teknolojia ya kisasa kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa VSOMO, unaowawezesha wanafunzi kujifunza kwa kutumia simu janja (smartphone) wakiwa mahali popote nchini.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya, Ofisa Habari na Uhusiano wa VETA, David Mpondyo, alisema mfumo huo utasaidia kutoa fursa kwa watu wengi kupata mafunzo ya ufundi stadi bila kulazimika kuwepo darasani.
“Mwanafunzi anapakua programu ya VSOMO kupitia Play Store, kisha anaanza kujifunza kwa nadharia kupitia simu yake janja. Baada ya kukamilisha sehemu ya nadharia, hufanya mafunzo kwa vitendo (practical) katika chuo cha VETA kilicho karibu na anapomaliza hupewa cheti kinachotambulika sawa na wale waliopo darasani,” alisema Mpondyo.
Alibainisha kuwa mfumo huo umetumika kwa zaidi ya miaka tisa na umeendelea kuboreshwa ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha hata sehemu ya vitendo inaweza kufanyika kwa kutumia simu janja.
Aidha, Mpondyo alisema VETA inatumia mfumo mwingine wa elimu kwa masafa uitwao Open and Distance e-Learning (ODeL), unaotumia TEHAMA kuwafikia wanafunzi walioko mbali na vyuo. Alisema mfumo huo unahusisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa kama Uhalisia Pepe (Virtual Reality), Vifaa vya kuiga mazingira halisi ya kazi (Simulators), Mechatronics, Roboti (Robotics), Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI) na Mtandao wa Vitu (Internet of Things – IoT).

Kwa mujibu wa Mpondyo, Serikali imetumia Shilingi milioni 273 kununua vifaa vya kufundishia vya kuiga mazingira halisi ya kazi (simulators) kwa ajili ya mafunzo ya uchomeleaji na uungaji vyuma, ili kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi.
Alisema kuwa mafanikio ya matumizi ya teknolojia hizo yameongeza ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia miongoni mwa wakufunzi, wanafunzi na wahitimu wa vyuo vya VETA, ambao wamekuwa wakibuni suluhisho la changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi kupitia maarifa waliyojifunza.
“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira. Tunaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo ili kufikia vijana wengi zaidi na kuwapa maarifa ya kisasa,” alisisitiza Mpondyo.
No comments:
Post a Comment